2012-12-17 08:07:13

Wajibu na dhamana ya Familia za Kikristo katika kulinda, kutetea na kudumisha utamaduni na ustaarabu unaoheshimu utu, maadili na dhamiri nyofu


Kardinali Vingt-Trois, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, hivi karibuni amezungumzia kuhusu ndoa na umuhimu wa familia katika maisha ya kijamii, kama njia ya kuanzisha mchakato unaopania kujenga ustaarabu mpya unaojikita katika mapendo thabiti kati ya mwanaume na mwanamke. RealAudioMP3

Amegusia hali halisi ya maisha ya ndoa na familia nchini Ufaransa, yanayoendelea kubadilika kwa kasi ya ajabu. Utu na heshima ya mwanadamu havina tena kipaumbele cha kwanza katika mabadiliko haya. Mwenyezi Mungu katika busara yake, alimuumba mwanamume na mwanamke, ili waweze kutegemezana na kukamilishana na kwa njia hii, waweze kuendeleza ile kazi ya uumbaji ambayo alimkabidhi mwanadamu, tangu kuumbwa kwa msingi wa ulimwengu.

Tangu mwanzo wa mapokeo ya Kiyahudi na Kikristo ndoa imekuwa ikiheshimiwa kutokana na utakatifu wake. Ni kwa njia ya ndoa, Mwenyezi Mungu alifunga agano na mwanadamu, ili kuendeleza ile kazi ya uumbaji inayofanywa na wazazi yaani Bwana na Bibi na wala si vinginevyo! Mtoto ni zawadi na tunda la uhusiano wa dhati kati ya Bwana na Bibi. Mwelekeo wa kupendana kati ya watu wa jinsia mbili tofauti ni sehemu ya mpango wa Mungu unaofanyika kwa kuzingatia uhuru wa watu husika pasi na shuruti.

Muungano kati ya Bwana na Bibi ndani ya Kanisa unaitwa Sakramenti inayowapatia watu hawa dhamana na wajibu mbele ya Kanisa na Jamii. Wanapaswa kutambua kwamba, ni muungano wa kudumu, hadi pale kifo kitakapowatenganisha kadiri ya mpango wa Mungu. Wanandoa wanaweza kuwa ni vyombo vya kudumisha haki, amani na utulivu ndani ya Jamii, ikiwa kama kila upande utatekeleza wajibu wake barabara.

Familia iwe ni mahali ambapo watoto wanajifunza tunu bora za maisha ya kiroho, kiutuu, kijamii na kitamaduni. Ni nguzo thabiti ya Jamii katika utekelezaji wa majukumu yake ya malezi na majiundo makini. Ndani ya Familia, watoto wanapaswa kupendwa na kuthaminiwa kama walivyo! Kuna uhusiano wa pekee kabisa kati ya wazazi na watoto wao unaobubujika katika maisha ya kibayolojia. Hapa ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ndani ya Familia unaozaa maisha kama zawadi inayopaswa kupokelewa na kuthaminiwa.

Kardinali Vingt-Trois anasema, upendo wa maisha ya ndoa ni kielelezo cha pekee kabisa cha agano kati ya Mungu na watu wake. Manabii walitumia lugha ya upendo wa maisha ya ndoa, kuelezea upendo ambao Mwenyezi Mungu aliuonesha kwa watu wake na hatimaye, kuthibitishwa na Kristo aliyeanzisha Sakramenti ya Ndoa kwa ajili ya Kanisa lake. Mwanaume na mwanamke wanashiriki katika agano na Mwenyezi Mungu.

Ikiwa kama mwanadamu anataka kufuta dhana hii, kwa hakika hatekelezi ule mpango wa Mungu kwa maisha na ustawi wa mwanadamu. Upendo wa kibinadamu ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu, kiini na chemchemi ya Familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Mabadiliko ya sheria za nchi zinazoruhusu watu wa jinsia moja kuoana ni jambo nyeti kabisa kwani linagusa undani na uhuru wa Mungu na binadamu katika ujumla wao.

Ni kielelezo cha mmong’onyoko wa maadili na utu wema. Kanisa linaposimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, linajikita zaidi katika uzazi na dhamana ya kuendeleza kizazi sanjari na dhamana ya watoto ndani ya Jamii. Kanisa linapinga uzalishaji wa watoto kwa njia ya maabara kwani linapenda wazazi kuwajibika barabara katika tendo la ndoa ambalo ni takatifu na lina umuhimu wa pekee kwa wanandoa wenyewe.

Kardinali Vingt-Trois anasema, Kanisa halina mpango wa kuendesha vita vya kisiasa dhidi ya sera zinazotaka kuleta mabadiliko kwa ajili ya kutetea asilimia mbili ya watu wanaounga mkono ndoa za watu wa jinsia moja. Kanisa linasukumwa na dhamiri nyofu, utu na heshima ya mwanadamu, linawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kusimama kidete kutoa mawazo ya dhidi ya utamaduni unaotaka kupinga mpango wa Mungu.

Watu wanapenda kukumbatia mno malimwengu na kwamba, Familia kwa sasa inaonekana kuwa ni kero kwa baadhi ya watu! Ni wajibu wa Familia za Kikristo kusimama kidete kulinda na kutetea tunu bora za maisha ya kifamilia ili kudumisha utamaduni na ustaarabu unaoheshimu utu, maadili na dhamiri nyofu.








All the contents on this site are copyrighted ©.