2012-12-17 08:00:14

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto zake Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania


Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, bila kusahau kumbu kumbu ya miaka ishirini tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni kipindi cha neema na Baraka kwa Familia ya Mungu Jimboni Mbeya. RealAudioMP3

Ni fursa ya kujenga na kuimarisha upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa Familia ya Mungu, ili kwa pamoja waweze kukuza na kuimarisha Imani ambayo, kimsingi wanapaswa kuitolea ushuhuda makini, kwa kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaifahamu Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya: Maandiko Matakatifu, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini wakiyajua kwa kina yaliyomo kwenye Nyaraka zote hizi, kwa hakika, watakuwa na nafasi ya kutolea ushuhuda makini wa Imani yao, bila kuifahamu Imani, si rahisi kwa waamini kuitetea na kuitolea ushuhuda.

Katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, Mama Kanisa anaendelea kuhimiza waamini kutolea ushuhuda wa Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kuanzia katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, lakini zaidi kwa njia ya Familia ya Watu wa Mungu, inayotembea pamoja katika maisha na utume wake. Ni kipindi cha kurudi tena katika ile ahadi ya Ubatizo, pale mwamini alipomkataa Shetani na mambo yake yote; alipojivua utu wa kale na kujivika utu mpya, akawa ni kiumbe kipya kwa njia ya Maji na Roho Mtakatifu kwa kuifia dhambi.

Je, Waamini wameendelea kuwa kweli waaminifu kwa ahadi hizi? Kama hapana, basi, Kanisa limewawekea kiti cha maungamo, ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, changamoto kwa waamini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kujitahidi kupokea Sakramenti za Kanisa kwa moyo na uchaji; kwa kutambua na kushiriki kikamilifu kutoka katika undani wa mtu mwenyewe! Mwamini asigenishwe katika Imani yake! Aifahamu kwa undani na mapana yake, awe tayari kusimama kidete kuilinda na kuitetea hadi dakika ya mwisho ya maisha yake!

Baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema Askofu Chengula, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kiasi kwamba, leo hii dunia ni kama Kijiji. Kuna maendeleo makubwa ya kichumi yanayoonesha utajiri wa vitu, lakini kwa bahati mbaya: utandawazi unaendelea kuwatumbukiza wengi katika umaskini na hali ya kukata tama; wengi wanaendelea kukengeuka pamoja na kumong’onyoa misingi ya maadili na utu wema!

Kumeongezeka migogoro na kinzani za kidini na kijamii; yote haya ni matokeoa ya utandawazi. Yote haya ni matokeo ya mwanadamu kutompatia Mwenyezi Mungu na Mwanadamu kipaumbele cha kwanza katika mipango na mikakati yake ya maendeleo. Mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kuiongoza dunia kwa jeuri yake mwenyewe! Nyaraka kumi na sita za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, zinafafanua masuala yote haya kwa Mwanga wa Kiinjili.

Askofu Evaristo Chengula anabainisha kwamba, kutokana na kumong’onyoka kwa misingi ya maadili na utu wema, na kwamba, watu wanaendelea kukengeuka, kumbe, kuna haja ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa Imani na Kweli za Kiinjili. Ni wajibu wa kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda, kwani kuna mamillioni ya watu ambao bado hawajawahi kusikia Injili ya Kristo ikitangazwa kwao. Mwaka wa Imani ni muda uliokubalika wa kuonesha mshikamano wa dhati katika Kanisa kwa kuchuchumilia mambo ambayo kimsingi yanawaungaanisha Wakristo katika Kanisa, ili wote waweze kuwa wamoja na dunia ipate kuamini.

Uwe ni Mwaka wa kuimarisha shughuli na mikakati ya kichungaji kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kwa kufanya hivi, kwa hakika, Mwaka wa Imani utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha!










All the contents on this site are copyrighted ©.