Kanisa linatambua na kuthamini michezo kama sehemu ya majiundo makini, mahali pa kutambua
na kuthamini zawadi ya maisha na kusikiliza kwa makini!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu tarehe 17 Desemba 2012 alikutana
na kuzungumza na Kamati ya Michezo ya Olimpic ya Kitaifa, Italia, iliyoshiriki hivi
karibuni katika michezo ya Olimpic iliyohitimishwa mjini London, 2012 kwa kuwashirikisha
wanamichezo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama mahali pa ushindani wa ufundi,
uwezo na karama ambazo walizitumia ili kufanikisha mashindano hayo, pamoja na kutambua
uwezo wao unapoishia.
Baba Mtakatifu anawapongeza kwa ushindi mkubwa waliojipatia
wakati wa Mashindano ya Olimpic, kielelezo cha nidhamu ya hali ya juu inayoheshimu
mwili wa mwanadamu, kwa kuonesha pia mshikamano, furaha na mafanikio yaliyogeuzwa
kuwa ni sherehe ya wengi. Hiki ni kielelezo cha ukuaji wa binadamu, kwa kujikatalia,
kwa kujenga na kudumisha moyo wa uvumilifu, unyenyekevu ambao kimsingi ndiyo siri
ya ushindi ya wanamichezo.
Michezo haina budi kuonesha huduma kwa mwanadamu,
kwa kuheshimu sheria na kanuni za michezo, uelewa na mtazamo wa binadamu anayehitaji
kwa namna ya pekee, elimu, maisha ya kiroho na tunu msingi zinazovuka upeo wake wa
kibinadamu. Michezo ni fursa makini ya elimu na utamaduni inayomwezesha mwanadamu
kujifahamu na hatimaye, kufahamu maana ya maisha yake. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican wanabainisha kwamba, michezo ni mahali ambapo mwanadamu anafafanua maana
ya maisha, utu na uhusiano wake na wengine.
Hapa ni mahali pa mwanadamu kufanya
maboresho ya maisha yake, anajitajirisha kwa kufahamiana na wengine, kwa kusaidiana
pamoja na kuweka uwiano mzuri wa utu wake unaopania kujenga na kuimarisha uhusiano
wa kidugu kati ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Utamaduni wa michezo unajengeka
katika utu wa mtu, ni sehemu ya huduma kwa mwanadamu na wala si vinginevyo.
Mama
Kanisa anatambua na kuthamini mchango wa michezo kama sehemu ya elimu, majiundo makini
ya mtu, uhusiano pamoja na tasaufi, ndiyo maana Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza
kwa michezo katika viwanja vya Parokia zake; mahali pa kujifunza na kujenga udugu,
kutambua na kuthamini zawadi ya maisha; daima wakiwa makini kuthamini mpango wa Mungu
katika maisha na kusikiliza kwa umakini mkubwa nyakati za mazoezi.
Mazoezi
yanaweza kuwa ni fursa ya kujibu maana ya maisha. Michezo inamfunda mtu tunu msingi
za maisha ya kiutu, changamoto kwa wadau wa michezo kutolea ushuhuda wa tunu hizi
wanazozimwilisha katika michezo; kwa kushirikiana na familia na taasisi za malezi
na majiundo ya vijana bila kuwasahau wadau wengine katika michezo.
Kamwe wanamichezo
wasitafute njia ya mkato kwa kutumia madawa ya kuongeza nguvu; wale wanaoteleza na
kuangukia katika mawazo haya duni, wapokelewe na kusaidiwa. Maadhimisho ya Mwaka wa
Imani, iwe ni fursa kwa wanamichezo kujifunza pia mapambano ya maisha ya kiroho, kwa
kuhakikisha kwamba, wema unashinda ubaya; ukweli unatawala dhidi uwongo; upendo dhidi
yachuki na uhasama. Michezo iwe ni uwanja wa majadiliano ya kidini na wale wanaoamini
na wale wasioamini; pawe ni mahali pa kushirikishana furaha na magumu ya maisha kwa
watu kutoka katika tamaduni, lugha na mielekeo ya mbali mbali ya kidini.
Kuwa
Mkristo ni kupenda zawadi ya maisha, mazingira pamoja na kuwapenda jirani, hasa wale
wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa
kuwatakia wajumbe wa Kamati ya Olimpic Italia na wanamichezo wote kheri na baraka
kwa Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012.