Jubilee ya miaka 100 ya Imani Katoliki Kaskazini mwa Uganda ni changamoto ya kuendelea
kujishikamanisha na Kristo kwa njia ya ushuhuda makini!
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu
amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Uganda kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka Mia Moja ya Imani Katoliki, Kaskazini mwa Uganda, kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa wema na ukarimu aliowajalia waamini wa Kanisa Katoliki Uganda. Huu ni mchango
wa Taifa la Mungu katika kurithisha Imani ya Kanisa Katoliki kutoka kizazi hadi kizazi,
wakitekeleza agizo la Yesu kwenda duniani kote ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu.
Tangu wakati huo, waamini Kaskazini mwa Uganda walipokea imani iliyoletwa
kwao kwa njia ya Wamissionari, wakiimwilisha katika maisha na kuvirithisha vizazi
vingine vilivyofuata kwa njia ya Ibada. Huu ni mchako mkubwa uliotolewa na Makatekista
waliokuwa ni wasaidizi wakuu wa Wamissionari katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji.
Kuna wafuasi mbali mbali wa Kristo ambao wameonesha ushuhuda wa pekee kwa njia ya
maisha yao na kwamba, kwa damu yao imekuwa ni chemchemi ya Ukristo nchini Uganda.
Changamoto
kubwa inayowakabili waamini sehemu mbali mbali za dunia ni kuchuchumalia wongofu wa
ndani na utakatifu wa maisha kama wanavyohimiza Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa
Vatican na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni mjini
Vatican. Waamini wajitahidi kujipatanisha wao kwa wao pamoja na Mwenyezi Mungu kama
njia mpya ya uinjilishaji Mpya unaodai toba na wongofu wa ndani.
Kardinali
Filoni anaitaka Familia ya Mungu nchini Uganda kuimarisha Katekesi kuhusu Sakramenti
za Kanisa, hasa Ubatizo, Ekaristi takatifu na Kipaimara; Sakramenti ambazo zinamwingiza
mwamini katika Ukristo, tayari kuanza hija ya utakatifu wa maisha. Kanisa nchini Uganda
liendelee kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa wale ambao bado hawajabahatika kuisikia
na waamini waendelee pia kuyatakatifuza malimwengu kwa kuonesha ushuhuda wa kukutana
na Yesu anayewakirimia furaha tele katika imani.
Familia ya Mungu iendelee
kuwajibika kwa kuwatunza na kuwasaidia waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi; wahanga wa
vita na ubaguzi kwa kuwaoneasha kwamba, wana upendeleo wa pekee machoni pa Kristo.
Katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji Mpya, wakumbuke kwamba, hawako peke
yao, kwani Kristo ameahidi kuwa pamoja nao hadi ukamilifu wa dahali. Maadhimisho ya
Jubilee ya miaka mia moja ya Ukristo Kaskazini mwa Uganda iwe ni fursa ya kujishikamanisha
na Kristo katika adhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; wajitoe kimaso maso kutangaza
Habari Njema ya Wokovu ndani na nje ya mipaka ya Uganda.
Bikira Maria nyota
ya Uinjilishaji Mpya awalinde na kuwaongoza katika utekelezaji wa Uinjilishaji Mpya.
Ni mwaliko wa Majimbo ya Nebbi, Gulu, Lira na Arua kusimama kidete ili kutangaza matendo
makuu ya Mungu katika maisha na utume wao nchini Uganda.