Dhamana na majukumu ya wanawake katika maisha na utume wa Familia
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi chetu kilichopita tuligusia kuhusu
uwiano wa majukumu ya kiuchumi na malezi katika familia kati ya mume na mke. Tulimalizia
kusema mwanamume anapofanya kazi za kiuchumi nje ya familia awe na lengo la kuipatia
familia yake mkate au mahitaji yake ya kila siku. Hata hivyo ongezeko
la mahitaji ya leo lililoletwa na mabadiliko ya kiuchumi linaonyesha kuwa ajira ya
baba pekee yake haitoshi kwa mahitaji yote ya familia. Hivyo leo tunashudia alama
wazi kuwa mwanamke naye hana njia nyingine ila kujiingiza kwenye shughuli za ajira
na kiuchumi. Tendo hili halina ubaya wowote ila tunarudia tena kusema mwanamke
ni mama wa watoto lakini mke kwa mumewe. Kazi yoyote ya kiuchumi isije ikamtoa kwenye
majukumu haya, isije ikahatarisha umoja wa kindoa na kuwa pingamizi katika uzazi na
makuzi ya watoto ambayo kwa hakika mwanamke ndiye muhimili mkuu. Kwa bahati mbaya
wimbo la kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata wimbo la haki sawa kwa mwanamke linawafanya
wanawake wengi watamani na hata kufanya kila njia kujivua uanawake wao katika majukumu
ili wapate elimu ya juu, kipato cha juu na nafasi za juu katika ajira huku wakitupilia
mbali uzazi na malezi. Ni masikitiko makubwa kuwa nchi zilizoendelea zimejikuta kwenye
idadi ndogo ya watoto yaani kundi tegemezi. Kiuchumi inaonekana ni sawa kwani
ndio maendeleo lakini baadaye ya taifa iko wapi bila watoto? Baadhi ya mataifa yaliyoendelea
yamesituka na kuanza kampeni ya kuelimisha kuhusu umuhimu wa uzazi ila kwa kuchelewa
na sio kazi rahisi kutibu ugonjwa wa fikira. Nasikitika mitaala ya kufundishia
mashule ya nchi zetu zinazoendelea sasa inakazia kwamba njia sahihi ya kuondokana
na ogezeko la watu na hasa kundi tegemezi ni kupunguza uzazi hata kwa njia za mauaji.
Je, nasi hatajikuta kwenye hali kama hiyo? Maendeleo ya kichumi sawa lakini kuwe na
uwiano kati ya uchumi na familia na hasa nafasi ya mwanamke ambaye ndiye anayebeba
mimba na kuzaa. Jambo la msingi katika familia ni upendo na ushirikiano. Mume,
mke na watoto ni zawadi na tiba ya kisaikolojia kila mmoja kwa mwingine. Wakati wote
wana- familia wajitahidi kujenga mazingira ya furaha pamoja. Ikumbukwe pia kuwa, familia
ni zawadi kwa jamii nzima kwani ndio wanaounda jamii na ndio wateja wa haki, amani
na majukumu ya jamii nzima kumbe jamii katika maana ya serikali isaidie ustawi wa
familia. Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphael Mwanga, wa Jimbo
Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.