Changamkieni kilimo cha mazao mbadala ili kuinua kipato chenu!
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewataka wakazi wa wilaya mpya ya Mlele mkoani
Katavi walime mazao mbadala ya biashara kama alizeti, karanga na ufuta kwa sababu
yanachukua muda mfupi na hivyo kuleta kipato cha haraka. Ametoa wito huo Ijumaa, Desemba
14, 2012, wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nsenkwa mara baada ya kuweka
jiwe la msingi kwenye zahanati ya kijiji hicho akiwa katika siku ya pili ya ziara
yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi. Waziri Mkuu aliwataka
wakazi hao kuachana na mazoea ya kulima tumbaku kwa vile inachukua muda mrefu hadi
kukomaa na inachangia uharibifu mkubwa wa mazingira kwani inahitaji kuni nyingi wakati
wa kukausha. “Tumbaku hivi sasa haina bei kwa sababu wanaopanga bei ni wakubwa huko
nje... tuangalie mazao ya alizeti, ufuta na karanga kwa sababu yanatoa pesa kwa haraka
zaidi. Mfano mzuri ni Singida ambao wamekuja juu kiuchumi kwa sababu ya zao la alizeti,”
alisisitiza. Aliwataka wakazi hao waangalie ufugaji nyuki kama fursa ya kipekee
kwa sababu mkoa huo umejaliwa kuwa na misitu mingi na unaweza kuongeza kipato cha
mkoa wao. “Asali ni dawa, asali ni chakula, asali ni biashara na ina soko hapa nchini
hadi nje ya nchi. Changamkieni fursa hii, ongezeni uzalishaji wa asali na nta,” aliongeza.
Aliwashauri pia waangalie uwezekano wa kulima miembe ya kisasa kwa sababu inazaa kwa
wingi na katika kipindi kifupi mno. “Hii miembe yenu inazaa maembe 10-20 kwa mwaka
lakini ya kisasa inazaa hadi maembe 10,000, ikiwa chinichini tu,” alisema.
Akihimiza
kanuni bora za kilimo, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge waJjimbo la Mlele aliwataka waachane
na kilimo cha matuta na badala yake watumie kilimo cha sesa. “Ekari moja ya mahindi
inapaswa ikupatie magunia 20-25 ya mahindi, sasa wewe unalima ekari tatu na kuvuna
magunia 10, sababu kubwa ni nafasi zinazopotea kwenye miraba ya matuta, alisema. “Ni
lazima tuondokane na kilimo hiki kwa sababu hakina tija na tena kinatumia nguvu nyingi
na kupoteza eneo kubwa ambalo lingetumika kupanda mazao,” alisisitiza.