Miaka 40 ya WAWATA imekuwa ni ya Utumishi wa upendo kwa vitendo!
Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania, TEC, anawapongeza Wanawake Wakatoliki Tanzania wanapoadhimisha Miaka 40
ya utumishi kwa vitendo. Kipindi hiki kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 2012 ni safari
ndefu ya kujitakasa, kujiandaa na kutekeleza wajibu. Kutujuvya zaidi ni Padre Agapito
Mhando.
Ni kipindi
cha matumaini ya kusonga mbele licha ya magumu na changamoto nyingi. Ni kipindi cha
kukua na kukomaa katika: Imani, Matumaini na Mapendo, daima wakiendelea kumtegemea
Mwenyezi Mungu kama walivyofanya Waisraeli katika hija yao ya miaka arobaini Jangwani.
Ni mwaliko wa kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani, ili kupata neema na
baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Miaka 40 ya WAWATA, kimekuwa ni kipindi cha
huduma kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania. Wengi wameguswa na utume wa WAWATA wanaoendelea
kutumikia na kuwajibika kwa upendo wa Kristo. Ni wanawake wanaokubali, kuthamini,
kulinda na kutetea Injili ya uhai; kwa kulea, kushauri na kuelekeza watoto wao katika
kuchagua miito mbali mbali ndani ya Kanisa.
WAWATA imekuwa mstari wa mbele
katika kuwategemeza Waseminari na kuendelea kutangaza Injili ya Upendo kwa wahitaji
na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Kwa
hakika, miaka arobaini ya WAWATA imekuwa ni Injili kwa vitendo. Vita wameipiga, Imani
wameilinda, lakini mwendo bado hawajaumaliza, kwani utume wao bado unahitajika kwa
ajili ya wokovu wao binafsi na ulimwengu katika ujumla wake.