Unaweza kuishi vyema Mwaka wa Imani: kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na
Matendo ya Huruma!
@Pontifex, ndiyo akaunti ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika
mtandao wa kijamii unaojulikana kama Twitter, ambao siku ya kwanza ya kuzinduliwa
kwake, Jumatano, tarehe 12 Desemba 2012, saa 6: 00 umekwishapata wafuasi zaidi ya
millioni moja. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kujibu maswali makuu matatu yaliyochaguliwa
kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Swali la kwanza liliuliza ni kwa jinsi
gani mwamini anaweza kuadhimisha vyema Mwaka wa Imani katika maisha yake ya kila siku?
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita akasema "ni kwa kuzungumza na Yesu katika
Sala, kusikiliza kwa makini anayomwambia kutoka katika Injili na kumtafuta kati ya
wenye shida". Kwa maneno mengine tungeweza kusema, mwamini anaweza kuishi vyema Mwaka
wa Imani kwa njia ya Sala, Tafakari ya Kina ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma.
Swali
la pili liliuliza, Je, ni kwa jinsi gani Imani kwa Yesu inaweza kumwilishwa katika
ulimwengu usiokuwa na matumaini? Baba Mtakatifu anajibu kwa kusema kwamba, mwamini
akumbuke kwamba, hayuko peke yake. Mwenyezi Mungu ni mwamba thabiti ambao mwamini
anajenga maisha juu yake na upendo wake daima ni amini.
Swali la tatu aliloulizwa
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Je, ni ushauri gani unaoweza kuutoa ili
mtu aweze kuzama katika sala wakati ambapo amesongzwa na mambo ya kazi, familia na
malimwengu? Baba Mtakatifu anajibu kwa kusema kwamba "Yatolee kwa Mungu yote unayofanya,
omba msaada wake katika maisha yako ya kila siku na kumbuka kwamba, yuko daima pamoja
nawe".