Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya III ya Kipindi cha Majilio: Kanuni maadili katika
kuyatakatifuza malimwengu
Mpendwa mwana wa Mungu, tukiendelea kwa furaha katika Kipindi cha Majilio, leo tunaendelea
kulitazama Neno la Mungu kwa furaha ili tujifunze na kuonja upendo wa Mungu kwa njia
ya Neno wake. Ni Dominika ya III mwaka C, tukialikwa kufurahi kwa uchangamfu kwa maana
Bwana yu karibu.
Kama kawaida Dominika ya III ni Dominika ya furaha, kumbe
furahini katika Bwana. Katika Dominika hii tunatafakari Neno la Mungu pia tukimtazama
Mt Yosefu, Baba mlishi wa Bwana. Baba huyu anayosifa ya pekee ambayo kila mmoja wetu
anapaswa kuishikilia daima nayo ni UADILIFU. Mtakatifu Yosefu anamchukua Mama Maria
akiongozwa na Roho Mtakatifu na anafanya kazi ya kuitunza Famila Takatifu kama Mungu
alivyotaka.
Daudi anampa Yesu Kristo mahali pake katika nasaba ya Daudi. Mtakatifu
Yosefu ni yule ambaye anatufundisha kuwa wazi mbele ya maongozi ya Mungu, kutekeleza
mapenzi ya Mungu bila kuweka vikwazo na hivi kuruhusu mpango wa Mungu usonge mbele.
Mpendwa unayesikiliza Neno la Mungu basi jitahidini kuwa Yosefu mwingine katika familia
yako ili kazi ya Bwana isonge mbele.
Katika Somo la kwanza, Nabii Sefania anawaalika
Waisraeli kufurahi maana karibu Bwana atawaondoa katika utumwa na mateso yao na hivi
watarudi nyumbani. Kwa namna hiyo Nabii ataka kutufundisha uwepo wa Mungu kati yao.
Furaha hiyo ambayo anaitangaza Sefania ni furaha ambayo tulitangaziwa kwa njia ya
ubatizo, yaani tulipoondolewa katika mkanda wa dhambi ya asili na dhambi nyingine
zote. Ni furaha tunayoipata tunapotafakari Neno la Mungu kila siku katika jumuiya
zetu.
Ni furaha ya kuishi pamoja katika familia nje ya utumwa, maana katika
utumwa hakuna familia bali ufisadi unaodhulumu familia. Mpendwa nani anapenda kukaa
katika utmwa na uonevu usioisha? Basi ndugu yangu furahini katika Kristu anayekualika
kila siku kupokea toba na msamaha wa dhambi. Ili kufurahi lazima kuiga mfano wa Mt.
Yosefu mwadilifu na daraja la mapenzi ya Mungu.
Tunapotafakari somo la Injili
tunakutano na sura ya Yohane Mbatizaji ambaye anatoa mafundisho yake juu ya maisha
hasa yale yanayompendeza Mungu. Kuwasaidia walio maskini, kuacha dhuluma na shuru
zinazozidi kiwango stahili au pangwa na wanaohusika. Pateni mishahara inayolingana
na kazi zenu na walipaji wa mishahara walipe kadiri ya kazi yenyewe na maisha ya
wakati huo. Nabii anafundisha juu ya jamii jinsi ya kuishi kwa ustarabu tukimwelekea
Mungu. Mpendwa haya Je wayajua na wajaribu kuyaishi yaani ndiko kuishi Injili?,
Baada
ya Nabii kufundisha hayo ataendelea na mafundisho mengine juu ya Masiha ni nani? Anatufundisha
unyenyekevu na uadilifu uleule ambao Mt. Yosefu atufundisha. Yohane Mbatizaji anasema
waziwazi kuwa pamoja na haya yote anayofanya yeye si Masiha bali nio sauti ya mtu
aliaye nyikani akitayarisha watu wakaandae mapito ya Bwana. Tena akikazia jambo hilo
anasema yule ajaye ni mkuu kiasi hawezi kugusa hata kamba za viatu vyake. Masiha ajaye
ni mwenye nguvu ambaye atahukumu yote kwa haki.
Mpendwa mwaliko kwako ni uadilifu
na unyenyekevu, kujishusha mpaka sakafuni mbele ya Mungu, ndiyo kusema hivi leo Kristo
yu nasi kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi, kumbe kuabudu Ekaristi siyo uchaguzi bali
ndiyo namna ya kumwelekea Mungu na kukaa naye. Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe Yn
1:1 na hivi kulisoma na kulitafakari kwa upole na ustadi wa kiroho ni njia za kumtukuza
Mungu. Katika mwaka huu wa imani Baba Mtakatifu anatualika akisema Neno la Mungu ndicho
chakula cha Imani na chakula hiki huletwa kwa njia ya Kanisa Takatifu.
Kila
siku lazima kuitika na kujibu swali hili aliloulizwa Bwana “tufanye nini ili kutimiza
mapenzi ya Mungu? Bwana anajibu akisema “mwamini yule aliyetumwa naye” Yn 6:28-29.
Mpendwa kumwamini Mungu si kujua tu yaliyomo ndani ya imani bali kuyaishi na kuyaweka
katika maisha ya watu. Kumwamini Kristo ndiyo mlango wa IMANI.
Mtume Paulo
anapowaandikia wafilipi anaendelea katika Dominika hii ya furaha kukazia maisha ya
furaha ambayo ni tunda la uadilifu. Si uadilifu tu bali maisha ya sala, kuwa watu
wa kutoa shukrani kwa kila jambo tupokealo toka kwa Mungu na kwa wanadamu. Mt. Paulo
anasema mkifanya hayo vema, amani ya Mungu itawahifadhi mioyo yenu daima. Haya basi
yatutayarisha kwa kupokea furaha ijayo ambaye ni Masiha, Emanueli, Mungu pamoja nasi.
Nikutakie
heri na baraka tele za majilio na kipindi chote cha Noeli kiwe mwanga kwako kwa ajili
ya uzima wa milele.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako
na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.