2012-12-14 08:32:44

Kuna mamillioni ya watu duniani yanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na: vita, maafa asilia, kinzani na migogoro isiyokuwa na majibu!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, hivi karibuni, wakati akichangia hoja kwenye kikao cha mia moja na moja cha Baraza la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wahamiaji alisema kwamba, kuna jumla ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum zaidi ya millioni sabini na mbili, ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, maafa asilia, miradi ya maendeleo na kinzani za kisiasa ambazo Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kuzidhibiti.

Wimbi la wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, linahitaji jibu makini kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kuratibu, kuonesha ukarimu pamoja na kuwa na sera zinazotekelezeka. Hizi ni kinzani zinazosababishwa na watu mbali mbali na wakati mwingine, zinachangiwa na Serikali ambazo hazina utawala bora. Madhara ya kinzani hizi yanajionesha kwa namna ya pekee mijini, hali ambayo inahitaji kudumisha utawala wa sheria unaozingatia pia haki msingi za binadamu.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano kwani wahamiaji hawa wameachiwa peke yao kushughulikia hatima ya maisha yao. Kuna watu zaidi ya millioni saba na watu wasiokuwa na makazi maalum wapatao millioni kumi na tatu ambao kwa miaka kadhaa wamekuwa wakitafuta kupewa hifadhi kama wakimbizi, lakini juhudi hizi zimegonga mwamba.

Hii ni rasilimali watu ambayo ingeweza kutumika katika uzalishaji mali kwenye nchi wahisani badala ya kuonekana kana kwamba, ni kizingiti cha maendeleo, kutokana na sera tenge na kandamizi dhidi ya wahamiaji na wageni. Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati.

Askofu mkuu Tomasi anaunga mkono wazo la kuanzisha Mfuko wa Hifadhi ya Dharura kwa Wakimbizi, utakaotumika kujibu kwa haraka zaidi matatizo na changamoto zinazotokana na wimbi la wahamiaji na wakimbizi, mara zinapojitokeza. Kuna haja ya kuwa na mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo la wahamiaji na wakimbizi kwa kuangalia chanzo kikuu kinachopelekea watu kama hawa kuyakimbia makazi na nchi zao.

Wachunguzi wa masuala ya kijamii wanabainisha kwamba, umaskini na athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo makuu yanayopelekea watu wengi kuhama katika nchi zao wakitafuta fursa za kuboresha hali ya maisha yao. Mambo haya yasipoangaliwa kwa umakini mkubwa, wahamiaji wanaweza kujikuta wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, au wanapoteza maisha yao wakiwa njiani kutafuta malisho ya kijani kibichi.

Ikumbukwe kwamba, wahamiaji wameendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi zao licha ya matatizo na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo ugenini. Wamejijengea uwezo wa kujiamini katika harakati za kuboresha hali yao ya maisha kwa kufanya kazi bila kuchagua. Ni watu wanaochangia pia ustawi na maendeleo ya nchi wahisani. Tatizo kubwa linalojitokeza ni ukosefu wa sera makini katika kuwashirikisha wahamiaji katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu unabainisha kwamba, wahamiaji kimsingi ni rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo ya Jamii; wanachangia katika maendeleo na kamwe si kizingiti cha ustawi wa nchi wahisani. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba, haki msingi za wahamiaji na wakimbizi zinalindwa na kuheshimiwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.