Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameahidi kutoa trekta moja kwa ajili ya kikundi
cha vijana katika kata ya Ilunde ili waweze kuondokana na kilimo cha jembe la mkono
na waboreshe uchumi wa eneo hilo.Ametoa ahadi hiyo Ijumaa, Desemba 14, 2012, wakati
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ilunde kwenye uwanja wa shule ya msingi Ilunde
katika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Waziri
Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi alisema atawapatia trekta hilo kama mkopo
ili nao wakirudisha trekta jingine, liweze kukopeshwa kwa kikundi kingine. “Hapa naanzisha
‘Kopa trekta lipa trekta’. Litakuja likiwa na jembe lake pamoja na harrow,” alisema
Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
“Ni lazima tuondokane na kilimo cha jembe la
mkono kwa sababu hakina tija... na zaidi nasisistiza kuondokana na kilimo cha matuta
kwa sababu kinatumia nguvu nyingi na kupoteza eneo kubwa ambalo lingetumika kupanda
mazao,” alisisitiza. Waziri Mkuu alielezwa matatizo yanayowakabili wakazi hao yakiwemo
ubovu wa barabara ya kutoka Inyonga (km. 60) na ukosefu wa wauguzi wa kike kwa ajili
ya akinamama wajawazito. Pia waliomba kupatiwa minara wa mawasiliano ya simu kwa sababu
wanapotaka kupiga simu, wanalazimika kupanda mti mmoja tu ambao uko km.12 kutoka kijijini
hapo.
Akijibu maombi yao, Waziri Mkuu aliwaita Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda
na Mhandisi wa Wilaya hiyo ili watoe maelezo kwa wananchi hao. Kuhusu wauguzi, mganga
mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Emmanuel Kamgobe alisema wanashugulikia suala hilo. Naye
Mhandisi wa wilaya hiyo, Injinia Godfrey Majuto alisema katika mwaka ujao wa fedha,
wilaya imetenga sh. Milioni 60 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Inyonga – Ilunde
na wameainisha kilometa tano ambazo ni korofi zaidi.
Mchana huu Waziri Mkuu
alifungua bweni la wasichana kwenye shule ya sekondari ya Ilela ambalo lina uwezo
wa kuchukua wanafunzi 52. Ujenzi wa bweni hilo umegharimu sh. milioni 36/-. Naye mbunge
wa viti maalum mkoa wa Katavi, Dk. Pudenciana Kikwembe ameahidi kutoa vyandarua, mashuka
na mablanketi kwa ajili ya wanafunzi wote 52 wa kwanza watakaolala kwenye bweni hilo.
Jumamosi, Desemba 15, 2012 atakagua kituo cha afya cha Inyonga na kuzindua mradi wa
madawati kwa shule za tarafa ya Inyonga.