2012-12-14 09:03:47

Kanisa Katoliki Afrika ya Kusini linaandaa Kongamano la Kitaifa ili kujadili kuhusu Ugonjwa wa UKIMWI, miaka 30 baada ya kugundulika kwake!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake Dhamana ya Afrika, Africae Munus, anahimiza kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini, wenye njaa, wagonjwa hasa wenye virusi vya Ukimwi na Kifua Kikuu; wakimbizi, wageni na wahamiaji. Kanisa litaendelea kutoa mchango wake kwa kuzingatia Heri za Mlimani, ambo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake.

Miaka thelathini imekwisha gota tangu wanasayansi walipogundua virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ambao umeendelea kupukutisha maisha ya watu kila pembe ya dunia. Katika mapambano haya, Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 22 Januari, 2013 litafanya Kongamano ili kujadili kuhusu mchango wa Kanisa Katoliki Afrika ya Kusini, miaka thelathini baada ya kugunduliwa kwa Virusi vya Ukimwi, huko KwaZulu Natal.

Kongamano hili linatarajiwa kufunguliwa na Monsinyo Roberto Vitillo, mshauri maalum kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kutoka Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, atakayezungumzia kuhusu hali ya ugonjwa wa Ukimwi Kimataifa. Padre Agbonkhianmeghe Orobator, Kutoka Chuo cha Hekima, Nairobi, Kenya atazungumzia kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kwa Bara la Afrika.

Kardinali Wilfrid Napier atapembua kuhusu utekelezaji wa mikakati ya mapambano dhidi ya Ukimwi mijini. Askofu Kelvin Dowling atajielekeza zaidi katika utekelezaji wa mikakati hii vijijini ambako kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa Ukimwi.

Kongamano hili pamoja na mambo mengine litaangalia kwa undani kuhusu tasaufi, mwelekeo wa kihistoria, maadili katika mapambano dhidi ya Ukimwi; ushirikiano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; mchango wa wanaharakati wa kike katika mapambano haya; sera za upimaji wa virusi vya Ukimwi; Kanisa na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.







All the contents on this site are copyrighted ©.