2012-12-12 14:26:02

Yesu Kristo ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu unaoweka Agano Jipya na la Milele!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jumatano tarehe 12 Desemba, 2012 ametafakari kuhusu Ufunuo wa Mungu mintarafu mpango wa ukombozi. Maandiko Matakatifu yanaelezea maendeleo yake katika historia ya Israeli hususan katika matukio ambayo yalionesha kukombolewa kwa Waisraeli kutoka utumwani Misri na hatimaye, Mwenyezi Mungu akaweka Agano lake.

Kwa karne nyingi Israeli imeendelea kusherehekea matukio ya kukombolewa kwake kutoka utumwani kwa njia ya Manabii; wakajifunza kuangalia mbele kwa matumaini ya kuwa na Agano Jipya na la Milele litakalowajumuisha watu wote. Mpango huu wa Mungu umejidhihirisha taratibu na kufikia hitimisho lake kwa ujio wa Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema katika kipindi hiki cha Majilio kutafakari ufunuo wa mpango wa Mungu juu ya ukombozi wa mwanadamu na kuendelea kutambua kwamba, kwa njia ya Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwa karibu zaidi na binadamu.

Licha ya ukosefu wa umakini na watu kuchukulia mambo juu juu tu bila kuzama katika undani wake, Baba Mtakatifu anawataka waamini kujifunza kutoka katika: imani, matumaini na mapendo; kutambua na kuzaa matunda ya uwepo wake, kwa kuwashirikisha wengine mwanga na furaha iliyoujaza mji wa Bethlehem.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alitambua uwepo wa Masista wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, walioweka nadhiri zao hivi karibuni. Anawaalika waamini kutafakari kwa kina, Maandiko Matakatifu, ili yaweze kuwa ni chachu ya ushuhuda endelevu wa Mungu kati ya watu wake. Waamini wajifunze kumtambua na kumpokea ili mwanga wake uweze kuyaangazia maisha yao.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 12 Desemba, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, msimamizi wa Amerika na nyota ya Uinjilishaji Mpya. Anawasihi vijana kujifunza kupenda na kutumaini kutoka katika shule ya Bikira Maria. Wagonjwa wafarijiwe kwa sala na maombezi ya Bikira Maria na kwa wanandoa wajiweke mikononi mwa Bikira Maria katika hija ya maisha yao ya ndoa.







All the contents on this site are copyrighted ©.