Tanzania inajiandaa kujenga hospitali kubwa zaidi 2013
Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwenye makabidhiano
ya majengo ya hospitali za Mnazi mmoja, Sinza na Rangi tatu, Jumanne, tarehe 11 Desemba
2012.
Nakushukuru sana Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Mkoa wa Dar es Salaam
kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika tukio hili muhimu la makabidhiano ya majengo
yatakayotumika kama vituo vya kutolea huduma ya afya kwa akina mama wajawazito na
watoto katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Sinza na Mbagala Rangi Tatu. Pamoja na majengo
hayo leo tutakabidhiwa pia magari matatu ya wagonjwa na vifaa tiba vya kisasa kwa
ajili ya kutolea huduma kwenye vituo hivyo. Hii ni hatua kubwa katika jitihada za
Serikli yetu za kuboresha afya za akina mama na watoto katika mkoa wa Dar es Salaam.
Sasa tumeongeza uhakika wa kupata huduma zilizo bora zaidi kutoka kwenye vituo hivi.
Kwa
niaba ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na wananchi wote kwa ujumla,
napenda kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Lee-Myung-bak, Rais wa Jamhuri ya Korea
(Korea Kusini) pamoja na serikali yake kwa zawadi hii kubwa waliyotupatia. Sina shaka
ye yote kuwa vituo hivi vitasaidia juhudi zetu za kupunguza vifo vya kina mama wajawazito
na watoto. Hatuna neno zuri la kushukuru isipokuwa kusema asanteni sana.
Gharama
zote za mradi huu, ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa na mafunzo kwa watoa huduma,
ni shillingi bilioni 6.76 fedha ambazo ni msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea.
Kabla ya msaada huu vituo vilikuwa havina magari ya wagonjwa, huduma za uzazi, upasuaji,
na maabara zilikuwa hafifu na vyumba vya kutoa huduma vilikuwa vichache. Kwa jumla
mazingira ya kazi yalikuwa siyo mazuri sana na mambo yote hayo sasa yamerekebishwa
na huduma zinazotolewa ni bora kuliko ilivyokuwa mwanzo. Kwa kweli marafiki zetu hawa
wametuonesha upendo mkubwa na urafiki usio kifani. Bila shaka wamethibitisha ule usemi
usemao: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Ndugu wananchi;
Tangu
nchi yetu ipate uhuru mwaka 1961 na kufanya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, Serikali
yetu katika awamu zote imefanya na inaendelea kufanya juhudi kubwa za kuboresha huduma
ya afya ili iwafikie Watanzania wengi zaidi na kwa gharama nafuu. Serikali ya Awamu
ya Nne ilipoingia madarakani mwaka 2005 iliendeleza juhudi hizo bila ajizi. Tulianza
kwa kuipitia upya Sera ya Afya ya Mwaka 1990 kwa lengo la kuihuisha ili iendane na
changamoto za sasa zinazoikabili sekta ya afya. Matokeo ya zoezi hilo ni kuasisiwa
kwa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi
(2007-2017), kwa kifupi MMAM.
Ujenzi wa vituo hivi ni matokeo ya utekelezaji
wa Mpango huo kabambe wenye lengo kuu la kuongeza kasi ya uendelezaji na uboreshaji
wa huduma ya afya kwa kujenga na kuimarisha hospitali, vituo vya afya na zahanati
nchini. Kazi hiyo tumeianza na tunaendelea nayo vizuri. Tunataka watu wasitembee zaidi
ya kilomita tano kufuata huduma ya afya. Aidha, tunaendelea kuboresha huduma zinazotolewa
katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Rufaa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tunafanya
hivyo nchi nzima kwa kushirikiana na wananchi, mashirika ya kijamii hasa ya dini,
watu binafsi na washirika wetu wa maendeleo waliopo ndani na nje ya nchi yetu. Ndugu
wananchi;
Wote mtakubaliana nami kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una changamoto ya pekee
katika utoaji wa huduma ya afya kwa wakazi wa Jiji. Mkoa wa Dar es Salaam una watu
wengi kuliko mikoa yote nchini. Kuna wagonjwa wengi kutoka hapa Mkoani na wengi huja
ama wenyewe au kuletwa Dar es Salaam kwa matumaini ya kupata huduma bora ya afya.
Hali hii inasababisha msongamano mkubwa katika hospitali za Serikali na za binafsi
zilizopo Jijini hapa.
Kwa kutambua ukweli huu na kwa nia ya kupunguza adha
wanayoipata wagonjwa, Serikali imekuwa inafanya jitihada kuongeza hospitali, vituo
vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Pia tunaongeza
vifaa tiba, majengo ya kutolea huduma na idadi ya wataalam wa afya. Kama nchi inayoendelea,
uwezo wetu si mkubwa sana kutosheleza mahitaji yote.
Hiyo ndio sababu
kubwa iliyonifanya mimi kuomba msaada Serikali ya Jamhuri ya Korea nilipoitembelea
nchi hiyo mwaka 2006. Bahati nzuri wakakubali kutujengea majengo haya tunayokabidhiwa
leo yenye maabara za kisasa na kutuongezea vifaa tiba vya kisasa na magari matatu
ya wagonjwa. Ndugu zetu hawa pia wametupatia mkopo ambao tunajenga hospitali kubwa
ya kisasa kule Mloganzila, Kinondoni. Hospitali hiyo itatoa huduma na kutumika kufundishia
wanafunzi wa udaktari, uuguzi na taaluma nyinginezo za afya. Tumeamua kukijengea
Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili makazi yake mapya pale Mloganzila ili kuongeza uwezo
wa kufundisha wanafunzi wengi zaidi ili tujitosheleze kwa mahitaji ya wataalamu wa
afya.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Ni kweli, ukilinganisha na tulivyokuwa
huko nyuma, kwamba tumepiga hatua nzuri kufikia Malengo ya Millenia ya Umoja wa Mataifa
ya kupunguza vifo vya watoto na akina mama vinayotokana na matatizo ya uzazi. Idadi
ya vifo vya watoto wachanga imepungua kutoka 99 mwaka 1999 hadi 51 mwaka 2010 na vifo
vya walio chini ya miaka mitano imepungua kutoka 147 hadi 81 kwa kila watoto 1,000
wanaozaliwa hai. Kwa upande wa akina mama wajawazito idadi ya vifo imepungua kutoka
578 hadi 454 kwa kila uzazi salama 100,000. Lakini wastani wa watoto 562 (wachanga
na walio chini ya miaka mitano) na akina mama 23 kufariki kila siku ni kubwa mno.
Tunaweza kupunguza zaidi vifo hivyo. Ni vifo vinavyoweza kuepukika kwa kuongeza
vituo vya kutolea huduma ya mama na watoto na kuboresha huduma itolewayo kama tufanyavyo
leo. Hivyo nawaomba wadau wote wajitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi za Serikali
za kupanua na kuboresha huduma ya afya nchini. Hii itawafanya Watanzania wawe na
afya bora na kuwezsha nchi yetu kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka
2015. Ushirikiano wa wadau wote ni muhimu sana katika kufanikisha azma hii. Hapa
nina maana ya Serikali, wananchi, watu binafsi na washirika wetu wa maendeleo kama
tufanyavyo leo. Tukiiachia Serikali pekee itachukua muda mrefu.
Napenda
kutumia nfasi hii kurudia wito wangu niliowahi kuutoa mwaka 2007 kwa Manispaa zote
tatu za Dar es Salaam kujenga hospitali na vituo vya afya vikubwa katika maeneo yao
mbalimbali ili kuzipunguzia mzigo hospitali zilizopo sasa za Temeke, Amana na Mwananyamala.
Hali kadhalika narudia wito wangu kwa Halmashauri za Miji ya Makao Makuu ya Mikoa
kujenga hospitali zao ili kuiacha hospitali ya Mkoa iwe ya Rufaa kwa Wilaya zote za
Mkoa husika. Mimi na wenzangu serikalini tunaahidi kutoa ushirikiano kwa wadau wote
ili kuhakikisha kuwa huduma ya afya nchini inazidi kuboreka. Tunapenda kuona ahadi
yetu ya maisha bora kwa kila Mtanzania ambapo upatikanaji wa huduma bora ya afya ni
sehemu muhimu, inaendelea kutekelezwa.
Tutaendelea kuongeza fedha kwenye bajeti
ya serikali kwa ajili ya sekta ya afya ili vituo vya kutoa huduma viongezeke na kumudu
majukumu yao ipasavyo. Tutaendelea kuongeza nafasi za masomo kwa wataalam mbalimbali
wa afya ili idadi yao iongozeke na kuziba pengo lililopo. Kwa kufanya hivyo mfumo
wa utoaji wa huduma ya afya na miundombinu itaimarika zaidi na afya za watanzania
zitaboreka zaidi. Tuna imani kuwa vifo vya watoto na akina mama vitapungua zaidi;
magonjwa yatazidi kudhibitiwa na watu wengi watakuwa na uhakika wa kuishi maisha marefu
zaidi kuliko ilivyo sasa. Ndugu wananchi;
Sasa majengo haya katika hospitali
za Mnazi Mmoja, Sinza na Rangi tatu yamekamilika. Nawaomba akina mama watumie vituo
hivi kupata huduma ya uzazi salama. Waache kujifungulia majumbani, ni hatari kwa usalama
wa mama na mtoto. Lolote linaweza kutokea. Vilevile, nawaomba madaktari, wauguzi na
watumishi wengine wa hospitali hizi watunze majengo haya na kutumia vizuri vifaa tiba
na magari ya wagonjwa kwani bila ya kufanya hivyo baada ya muda si mrefu huduma zitadorora.
Halmashauri zitenge fedha za kutosha za uendeshaji wa hospitali, vituo vya afya na
zahanati zake. Mazingira ya kazi katika zahanati zetu hizo tatu yameboreshwa na vitendea
kazi na vifaa vimeongezwa. Hakuna sababu ya kushindwa kutoa huduma kwa kiwango cha
hali ya juu. Mshindwe wenyewe!
Kabla ya kumalizia napenda naishukuru tena
serikali ya Jamhuri ya Korea kwa msaada mkubwa waliotupatia. Balozi wao yupo hapa.
Namwomba atufikishie salamu na shukrani zetu nyingi kwa Rais na watu wa Jamhuri ya
Korea. Tunawashuru sana kwa ukarimu wao. Tunaomba tuendelee kushirikiana pamoja katika
kuboresha sekta ya afya na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa; Ndugu
wananchi;
Baada ya kusema maneno hayo machache, sasa nipo tayari kufanya kazi
iliyonileta ya kupokea majengo haya na kuyafungua rasmi. Asanteni kwa kunisikiliza.