Kanisa Katoliki Burundi lazindua rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi hivi karibuni limezindua rasmi Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu
wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa
kwa mara ya kwanza.
Maadhimisho haya yamefanyika kwenye Parokia ya Muyaga,
Jimbo Katoliki la Ruyigi, Burundi. Hii ilikuwa ni parokia ya kwanza kabisa kuwapokea
na kuwakaribisha Wamissionari wa kwanza walipofika nchini humo ili kutangaza Habari
Njema ya Wokovu.
Maaskofu Katoliki Burundi wanasema, Mwaka wa Imani kiwe ni
kipindi cha kumwilisha Imani katika matendo, sanjari na ujenzi wa maeneo ya kumbu
kumbu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. Waamini
wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu ya Familia ya Mungu inayowajibika, changamoto
ya kujishikamanisha na kweli za Kiinjili, ili kujenga na kudumisha umoja, amani, upendo
na mshikamano wa kitaifa.
Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kujitaabisha
kuifahamu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, ili waweze kuitolea ushuhuda Imani wanayoungama
katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; Imani wanayoadhimisha katika Sakramenti mbali mbali
za Kanisa; Imani wanayojitahidi kuiishi kwa kufuata Amri za Mungu dira na kielelezo
cha matendo adili pamoja na Imani wanayoisali.