Askofu mkuu Ambrose Madtha kuzikwa India tarehe 14 Desemba 2012
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa
habari za kifo cha Askofu mkuu Ambrose Madtha aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Pwani
ya Pembe, kilichotoea tarehe 8 Desemba 2012 kwa ajali ya gari nje kidogo ya mji wa
Abijan.
Baba Mtakatifu ametuma salam za rambi rambi kwa Askofu mkuu Salvatore
Pennacchio, Balozi wa Vatican nchini India, ili aweze kumfikishia salam zake za rambi
rambi kwa familia, ndugu na jamaa ya Marehemu Askofu mkuu Madtha. Ni kiongozi aliyejitoa
kwa ajili ya kudumisha amani na kutafuta mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anaungana
na wote walioguswa na msiba huu mzito katika kipindi hiki cha maombolezo.
Wakati
huo huo, Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican anaungana na wote wanaomboleza
msiba huu uliotokea kwa ajali ya gari wakati alipokuwa anatoka kwenye maadhimisho
ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Anamweka marehemu Askofu mkuu
Madtha chini ya maombezi ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili aweze kumwombea
huruma na hatimaye, kupata tuzo la maisha ya uzima wa milele kutokana na utume wake
wa Kipadre.
Marehemu Askofu mkuu Ambrose Madtha anatarajiwa kuzikwa kijijini
kwake Belthangady, India, Ijumaa tarehe 14 Desemba, 2012. Mwili wa Marehemu Askofu
mkuu Ambrose Madtha unatarajiwa kuwasili nchini India Alhamisi tarehe 13 Desemba 2012.
Rais
Alassane Outtara wa Pwani ya Pembe ni kati ya viongozi na waamini waliotuma
salam zao za rambi rambi kutokana na msiba huu, kwani Marehemu ni kiongozi aliyejitoa
mhanga kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa upatanisho, haki na amani nchini Pwani
ya Pembe, iliyojikuta katika kinzani na vurugu za kisiasa. Baada ya vurugu zote hizi,
alisema, vita imekwisha sasa ni wakati wa kujenga misingi ya haki, amani, upendo na
mshikamano wa kitaifa, kila mtu akitekeleza wajibu wake.
Mkakati uwe ni kupania
kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi maadui makubwa ambao wanaoweza kulitumbukiza
taifa katika kinzani na misigano ya kivita. Wananchi wote wa Pwani ya Pembe, wakiwa
wameungana na kushikamana; haki msingi za binadamu zikiheshimiwa na kuthaminiwa; hapo
kuna kila sababu ya kusonga mbele kwa maendeleo endelevu.