2012-12-11 10:10:17

Mzee Madiba bado amelazwa! Wengi wanamwombea ili apone haraka!


Mzee Nelson Mandela Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini amelazwa kwenye Hospitali ya Kijeshi mjini Pretoria kwa ajili ya kuchunguza afya yake na kwamba, kuruhusiwa kwake kutoka hospitalini hapo kutategemea matokeo ya uchunguzi unaoendelea kufanywa ili kubaini kile kinachomsumbua kwa sasa.

Hayo yamesemwa na Bi Nosiviwe Mapisa-Nqakula, Waziri wa Ulinzi nchini Afrika ya Kusini, baada ya kumtembelea Mzee Mandela mapema jumatatu tarehe 10 Desemba 2012. Anawaalika wananchi na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kumkumbuka Mzee Mandela katika sala zao, ili aweze kupona mapema na hatimaye, kuendelea na maisha yake ya kawaida. Kwa sasa anahitaji utulivu na mapumziko makubwa zaidi na hakuna sababu ya kubabaika. amekazia Bi Mapisa-Nqakula.

Wasi wasi ulianza kutanda miongoni mwa wananchi wa Afrika ya Kusini baada ya kimya kikuu kuhusiana na ugonjwa wa Mzee Madiba na kwamba, alikuwa anahudumiwa kwenye Hospitali ya Kijeshi. Umaarufu wa Mzee Mandela ndio unaowafanya watu wengi kutaka kufahamu maendeleo ya afya yake. Ni kiongozi na mfano wa kuigwa katika mapambano ya kutafuta haki msingi za binadamu, uhuru wa kweli, amani na upatanisho.

Watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kutuma salam na matashi mema, ili Mzee Madiba aweze kupona haraka. Rais mstaafu Nelson Mandela ana umri wa miaka 94 tangu alipozaliwa.

Taarifa ya Serikali iliyotolewa siku ya Jumanne tarehe 11 Desemba 2012 inaonesha kwamba, Mzee Madiba anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na kwa sasa anaendelea vyema na tiba. Mzee Madiba alilazwa hospitalini tangu tarehe 8 Desemba 2012.







All the contents on this site are copyrighted ©.