Maboresho ya uhakika na usalama wa chakula Ukanda wa Sahel yanakwenda sanjari na amani
na utulivu!
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO Bwana Josè
Graziano da Silva hivi karibuni amesema kwamba, maboresho ya uhakika na usalama wa
chakula Ukanda wa Sahel yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa amani na utulivu katika
Ukanda huu ambao kwa miaka ya hivi karibuni umekuwa ni Uwanja wa Mapambano.
Bwana
Da Silva ameyasema hayo wakati akichangia mada kwenye mkutano uliokuwa umeitishwa
na Professa Romano Prodi, Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ukanda
wa Sahel, Kaskazini mwa Afrika. Maboresho ya sekta ya kilimo ni mtaji mkubwa unaoweza
kusaidia mchakato wa kudumisha amani na utulivu, kwani kuna uhusiano wa karibu sana
kati ya baa la njaa na kinzani za kivita; usalama wa chakula na amani Barani Afrika.
Ukanda
wa Sahara unakabiliwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa usalama wa chakula, baa la njaa
na umaskini na matokeo yake, rasilimali kidogo iliyopo imekuwa ni chanzo cha kinzani
na migogoro katika eneo hili. Usalama wa chakula unakwenda sanjari na usalama pamoja
na maendeleo endelevu. Jumuiya ya Kimataifa imekwishachangia kiasi cha Billioni moja
za Euro katika kipindi cha mwaka huu na baa la njaa linaendelea kudhibitiwa kwa kiasi
kikubwa.
Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na mikakati ya muda mfupi
inayogusa kwa namna ya pekee: usalama wa chakula na lishe; afya, elimu pamoja na
usalama. FAO inaendelea kujizatiti kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wengine wa
maendeleo na misaada Barani Afrika ili kupata maendeleo ya kweli katika Ukanda wa
Sahel.