2012-12-08 10:59:50

Tafiti zinaonesha kwamba, Wakristo wanadhulumiwa sana sehemu mbali mbali za dunia!


Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, akishiriki katika mkutano wa ishirini na tisa wa Baraza la Mawaziri wa Shirikisho la Usalama na Maendeleo Ulaya, OSCE, uliofanyika hivi karibuni huko Dublin, Ireland, amekazia umuhimu wa uhuru wa kidini kati ya nchi wanachama wa Shirikisho hili.

Anasema, Vatican katika vipaumbele vinavyohusu uhuru, inatoa kipaumbele cha kwanza katika uhuru wa kidini. OSCE kwa upande wake, imeendelea kutambua mchango madhubuti unaotolewa na Jumuiya na Mashirika ya Kidini ndani ya Jamii husika. Kutokana na mwelekeo huu, OSCE inatambua na kuthamini mawazo na mwono wa kidini unogusa kwa namna ya pekee: Madhehebu, Ibada, Elimu, Upashanaji habari na uhuru wa mtu kuabudu dini anayopenda.

Askofu mkuu Mambert anasema kwamba, haki msingi zinazohusianishwa na mambo ya kidini zinahitaji kulindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa, ikionekana kana kwamba, uwepo wake unaendelea kuhatarishwa kutokana na misimamo ya kisiasa au ubaguzi unaofanywa wakati mwingine kwa misingi ya kidini. Uhuru wa kuabudu hauwezi kujieleza kwa njia ya Ibada peke yake, bali unapaswa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kutoa fursa kwa waamini kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Jamii yao.

Kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya kutovumiliana miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani; imegundulika kwamba, Wakristo ni kati ya wanaodhulumiwa kwa kiasi kikubwa hata miongoni mwa nchi wanachama wa OSCE. Licha ya mikakati na sera ambazo zimechukuliwa na Nchi wanachama wa OSCE, bado hakuna uvumilivu, kuna sheria baguzi, maamuzi, tabia kwa njia ya matendo au kwa kutotimiza wajibu; mambo ambayo yanaondoa uhuru wa kuabudu.







All the contents on this site are copyrighted ©.