2012-12-08 08:53:31

Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili "Kweli Bwana ameufunua ukombozi wake machoni pa mataifa ameonesha haki yake"


“Atukuzwe Mungu…. Aliyetuchagua kabla ya kuumbwa ulimwengu”. Maneno haya ya mtume Paulo, yanatufumbulia ukweli mkuu kwamba: mwanzoni kabla ya uwepo wetu, kuna uchaguzi wa kimungu katika Kristo. Yaani, hatupo hapa ulimwengu kwa bahati nasibu, au kwa kufumuka tu kama uyoga, au kwa msukumo fulani wa lazima. La hasha. Binadamu kabla ya kuwepo hapa ulimwenguni tumefikiriwa, tumehitajika na tumechaguliwa na Mungu Baba “kabla ya kuumbwa ulimwengu.” RealAudioMP3


Leo tunaadhimisha mwanzo wa uwepo wa “Bikira Maria Immakulata”. Ina maana kwamba, uwepo wake ulifikiriwa, uliandaliwa, na kuchaguliwa na Kristu “kabla ya kuumbwa ulimwengu”. Ndugu zangu, budi ieleweke kwamba katika kuzaliwa hapa duniani, hakuna binadamu, anayemchagua na kumwandaa mama yake atakakotungwa mimba na tumbo atakalozaliwa, bali anashtukia tu amezaliwa kwa mama yeyote yule.

Mwingine unashtukia umezaliwa kwa mama mnene sana, mwingine kwa mama mwembamba; mwingine kwa mama kichaa, kwa mama wa kabila hili, kwa mama wa dini hii au ile kwa mama mbaya au kwa mama mwema, nk. Ni Yesu pekee aliweza kumwandaa mama yake wa kumzaa. Akamwumba na kumtengeneza vizuri, akamkinga na dhambi na kasoro zote. Mwumbaji anazaliwa kwa kiumbe chake. Ama kweli “Mwenye bahati habahatishi” Ndiyo bahati na neema ya uhakika aliyopata Mama yetu Bikira Maria.

Leo kwa imani yote kanisa linatufundisha jinsi kulivyokuwa asili au chanzo cha kukingwa dhambi ya asili huyu mzazi mtakatifu wa Mungu. Fundisho hilo la kanisa linathibitisha vipengele vikuu viwili: Mosi, kwamba Maria alikingiwa dhambi ya asili toka pale alipotungwa mimba; Pili, tendo hilo la kukingiwa dhambi ya asili ni tendo la huruma na ni la pekee sana la Mungu Baba litokanalo na mastahili ya Kristu. Yaani kutokana na Kristu tu, ndiyo Maria ameweza kukingiwa dhambi ya asili.

Ili kulielewa tendo hilo la ajabu la huruma na upendo wa Mungu kwa Maria kupitia kwa Yesu Kristu, tusome na kutafakari sana somo la kwanza. Somo hilo linaeleza vizuri juu ya mapato ya dhambi ya kwanza ya Adamu na Eva. Binadamu hao walipoteza neema ile ya utakatifu wa awali waliyopata. Kwa hiyo, walivunja urafiki wao na Mungu wakabaki kumwogopa Mungu aliyewaumba kwa sura na mfano wake.

Aidha umoja na uhusiano ule mzuri uliokuwapo kati ya mwanaume na mwanamke ukakorofika na kuwa katika ukinzani. Mwanaume akaanza kujiona mtawala wa mwanamke. Mapato ya dhambi iliyotendwa na binadamu wa kwanza haikuishia kwao tu. Adamu na Eva walitenda dhambi zao binafsi, lakini dhambi hiyo ikatunasa sisi binadamu wote yaani, dhambi ya kutoshiriki uzima wa Mungu, tulioshirikishwa sote ili kuwa na umoja naye. Dhambi hiyo inatutenga na binadamu wenzetu na kutufanya tusiishi kwa amani, kwa umoja na upendo na watu wote. Hiyo ndiyo hali yetu halisi.

Maria ni binadamu pekee, aliyekingwa, toka mwanzoni kabisa mwa maisha yake yaani, toka pale alipotungwa mimba hakuwa na doa lolote la dhambi. Huruma ya Baba ndiyo ilitimiliza tendo hilo la kuteuliwa na la kukingiwa dhambi Bikira Maria. Huruma ya Baba kwa nafsi hii ya Maria ni dhidi ya uovu unaomiliki ulimwengu, yaani, kule kumweka Maria juu ya kila uovu na dhambi ambayo budi kila mmoja wetu apambane nayo kutokana na hali halisi ya ubinadamu ulioanguka.

Maria alibarikiwa kwa baraka zote za kiroho kwa njia ya mwanae Kristo. “Nitaweka uadui kati yako na mwanamke”: maneno haya yanatimia kwa Maria. Toka alipotungwa mimba, amekuwa adui binafsi wa Shetani. Maria ni mpinzani wa shetani kwa vile hakuna uhusiano wala ushirikiano wowote katika kuujenga ufalme wa uovu. Maria ni mpambanaji wa kwanza dhidi ya dhambi.

Imani ya kanisa inatufundisha ukweli mwingine kuhusu mwanzo huu wa Maria, na kuhusu uteuzi huu wa pekee unaomkinga Maria na kila kosa na kumbariki kwa baraka zote na sadaka ya Kristu msalabani. Hili ndilo fumbo kuu kwetu tunaloweza kuliona leo ni kwamba kila adhimisho la kikristu, adhimisho la ukuu wa kazi ya ukombozi ya Kristo; ni neema ya msingi, ni neema safi na ya fahari kuu. Yaani, katika nafsi ya Maria, ukuu wa kifo na ufufuko wa Kristo unatukuka zaidi na unapata umuhimu wa pekee.

Mwenyeheri John Henri Newman anasema kwamba katika Maria, “Bwana amefunua ukombozi wake, machoni pa watu wake ameonyesha haki yake. Amemtendea Maria zaidi ya kile alichokifanya kwa binadamu wengine. Kwa wengine amewapa neema na uweza wa kuendelea kuanzia pale walipoanza kuishi hapa duniani: Kumbe kwa Maria alimpatia neema hiyo tangu mwanzo kabisa.” [J.H. Newman].

Ukweli huo unatoa mwanga kwenye usiku wa giza la fumbo la kibinadamu kwa hoja mbili: Kwa upande mmoja, katika Maria, sisi tunaweza kutambua siyo nani ni kipeo cha binadamu, bali tunatambua nani ni binadamu halisi. Yaani tunatambua hali halisi aliyokuwa nayo binadamu toka mwanzo kabisa mwa maisha yake, siyo suala la kidhahania (kimawazo tu) ambalo yabidi kulifuata, bali ni kitu halisi ambacho kinafanya uwepo wetu binafsi, na kinacholenga kwenye kuwa waana warithi kwa njia ya Yesu Kristu kadiri ya mapenzi ya Baba. Nje ya ukweli huu unaopinga mahusiano hayo na Kristu ni uwongo.

Kwa upande mwingine, kutokana na fumbo tunaloadhimisha leo, tunaweza kujitafiti kikamilifu maovu yetu ya kiroho na maovu yanayotawala ulimwenguni kutokana na dhambi ya asili. Ukweli wa dhambi ya asili ni ukweli ambao ni mgumu sana kuupokea, lakini kukataa au kusahau uwepo wa dhambi ya asili ndiyo unaofanya hali halisi ya kibinadamu kuonekana kuwa fumbo lisilotanzulika.

Kutotambua na kudharau kwamba hali halisi ya ubinadamu wetu ni tete, imejeruhiwa na ina mwelekeo wa kutenda uovu (unaosababishwa) au unaotokana na makosa ya kielimu, ya siasa, ya kijamii, ya kitamaduni, ya kidini nk. Mama wa Mungu, zaidi ya mtu mwingine yeyote, aliishi mang’amuzi ya fumbo hilo la ukombozi wa kibinadamu.

Katika maingilio ya adhimisho hili kubwa la fahari tunatambulishwa fumbo hilo kwa wimbo usemao:

Tota pulchra es Maria U mzuri kabisa Ee Maria.” Kwa mara nyingine tena tunapenda kukuangalia wewe, Ee Maria, ili kutafakari uzuri wa nafsi yako: Uzuri ambao unang’ara ukweli wa ubinadamu wewe. Katika wewe, sisi leo tunatekelezewa mradi wa Mungu ndani ya kila mmoja wetu. Mvuto unaoishi wewe, umetokana na ukweli kwamba mioyo yetu inaona ndani yako kutekelezwa kikamilifu matakwa na nia zako za uhalisia wa maisha.

Ubora wa ukombozi wa Kristu, ambao unadhihirika katika mng’aro kamili ndani yako, unadhihirika na kuonekana ndani ya historia ya kila siku ya maisha yetu. Inadhihirika katika utakatifu wa maisha ya watu wengi wanaoishi maisha yao ya sakramenti mbalimbali hususani sakramenti ya ndoa.

Yanadhihirika kwa wahitaji tunaoishi nao kila siku. Unadhihirika ndani ya watu wengi wake kwa waume wanaojitolea kila dakika kuwafundisha watoto na vijana katika familia zetu na mashuleni. Katika uaminifu na shujaa wa mapadre katika huduma za uchungaji. Huu ndiyo mwanga unaoangaza mahali maisha yetu na kila mahali tuishipo. Tusisahau pia kwamba, mwanga huo umezungukwa pia na giza; yaani mambo mengi yanayoukandamiza moyo pindi tunatafakari uzuri wake. Kwa mfano, hali ya watu kukosa kazi ni usiku unaotisha kwa wengi.

Wahusika wanawazibia wengine njia huru za ubunifu wa kiuchumi, badala ya kuwaacha watu huru kubuni njia zifaazo. Aidha, ni jambo la kutia huruma kwa vijana ambao waliokata tama kwa vile maisha yao yameharibika. Vijana wanaoonekana wakizurura mabarabarani, mitaani, vijiweni; au vijana wale ambao wamefilisika kiroho na ni watupu kabisa kwa sababu wamenyimwa haki yao ya msingi kabisa: yaani elimu. Yaani, kuelimishwa na wazazi wao, au na watu wakubwa, au ni vijana wanaopotoshwa na wengine, hivi wanashindwa kupambanua kati ya chema na kibaya, kizuri na kichukivu.

“Tunaukimbilia ulinzi wako,
Ee mzazi mtakatifu wa mungu,
Usikatae maombi yetu katika shida zetu,
Bali utuokoe siku zote katika kila hatari,
Ee Bikira mtukufu na mwenye baraka.
Ee Malkia wetu,
Ee Mshenga wetu,
Ee Mwombezi wetu,
Utupatanishe na mwanao,
Utupendekeze kwa mwanao,
Utukaribishe kwa mwanao,
Ee Bikira mtukufu na mwenye baraka. Amina.”

Tafakari hii imeandaliwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.