Mshikamano wa Papa Benedikto XVI kwa wananchi wa Ufillipini waliokumbwa na tufani!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi tarehe 8 Desemba 2012,
aliyaelekeza mawazo yake nchini Ufilippini, akionesha uwepo wake wa karibu kwa watu
waliokumbwa na tufani kubwa ambayo imesababisha maafa makubwa na watu wengi kwa sasa
wamelazimika kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Ni matumaini
ya Baba Mtakatifu kwamba, Imani na Upendo wa kidugu utakuwa ni nyenzo na nguvu ya
kuweza kupambana vyema na majaribu haya. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kuikimbia dhambi na nafasi zake, ili kutunza ile neema ya utakaso waliyoipokea
wakati walipobatizwa. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni kielelezo makini cha
ushirikiano wa neema ya Mungu.
Taarifa zinabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu
laki moja na sitini ambao hawana mahali pa kuishi na kwamba, nyumba zaidi ya elfu
moja na mia tatu sitini zimehabiwa vibaya na hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Baba
Mtakatifu mwishoni, amewabariki wanachama wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Italia ambao
wamerudia tena ahadi yao ya kutaka kujikita zaidi na zaidi katika utakatifu kwa kushirikiana
na viongozi na walezi wao kwa ajili ya azma ya Uinjilishaji Mpya.
Amewakumbuka
wafanyakazi wa sekta ya afya wanaotekeleza wajibu wao katika Hospitali za Kanisa ambao
kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu baada ya ruzuku iliyokuwa inatolewa kwenye hospitali
hizi kufutwa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ni matumaini yake kwamba,
wahusika wataweza kupata suluhu ya kudumu kuhusiana na tatizo hili.