2012-12-08 10:02:16

Mitandao ya Kijamii ni huduma mpya kwa Injili


Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii walipigwa na bumbuwazi waliposikia kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amejiunga na mtandao wa Twitter ili kuweza kutwitter pamoja nao. Baadhi yao walionesha kejeli, lakini wengine wakasema, kwa hakika inapendeza, tuangalie kama atakuwa na wafuasi wengi kama walivyo "vigogo" wengine duniani.

Watumiaji hawa walijikita zaidi katika idadi ya wafuasi badala ya kuangalia maudhui, hatimaye, baadhi ya watu wakasema, kwa hakika sasa "tumepata mtu atakayeipatia roho, kile inapenda". Pengine ni mapema mno kuweza kumhukumu, tukae kitako, tuone na kusikiliza mambo yatakwenda namna gani! Tutafurahia kutwitter pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wanaotafuta habari kwa njia ya mtandao. Mtandao huu utatoa matunda na kuongezeka zaidi kadiri ya udongo uliopo!

Hii ni sehemu ya Tahariri ya Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anayeangalia jinsi ambavyo watumiaji wa mitandao ya Jamii walivyopokea habari za Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kujiunga na mtandao wa twitter ambao unabeba maneno machache kabisa. Tangu mwanzo, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna watu wameguswa kwa maneno machache tu waliyoyasikia kutoka katika Maandiko Matakatifu; maneno haya yakawa ni dira na mwongozo wa maisha yao yote.

Jambo la msingi ni watu kutambua umuhimu wa maneno haya, chanzo na lengo lake ili kupata maana inayokusudiwa. Watumiaji wa twitter wanaweza kuupokea ujumbe huu au wakaamua kuubeza. Ni sawa na mbegu iliyoanguka katika udongo tofauti na kila udongo ukatoa matunda yanayokusudiwa.

Padre Lombardi anahitimisha tahariri yake kwa kusema kwamba, ulimwengu hauwezi kukombolewa kwa njia ya matumizi ya mitandao ya kijamii. Kwa njia hii, kuna mamillioni ya Wakristo watapata nafasi ya kumsikiliza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa njia ya mitandao hii; wakaonja uwepo wake wa karibu, ili kuruhusu hekima yake iweze kupenya na kugusa akili na nyoyo zao, ili kuweza kushirikishana na rafiki zao kwa njia ya mitandao.

Kwa hakika, matumizi ya mitandao ya kijamii ni huduma mpya kwa ajili ya Injili







All the contents on this site are copyrighted ©.