2012-12-08 14:41:30

Bikira Maria ni kielelezo cha neema na upendo wa Kristo kwa Kanisa lake analolisafisha na kulitakasa ili liweze kung'ara kwa utakatifu!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alikazia dhamana ya Bikira Maria katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani; zawadi ambayo imemwezesha kujitoa bila ya kujibakiza ili kushiriki katika kazi ya ukombozi, hii ni kutokana na imani thabiti mbele ya Mwenyezi Mungu, kama walivyobainisha Manabii katika Agano la Kale.

Kwa njia ya Bikira Maria, ahadi zilizotolewa kwenye Agano la Kale zinapata utimilifu wake. Ameonesha usikivu mkubwa wa Neno la Mungu, akalipokea na kulikubali kiasi kwamba, Neno wa Mungu akafanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Kwa njia ya Bikira Maria ubinadamu na historia vinamfungukia Mwenyezi Mungu na hivyo, kuwa tayari kupokea neema na kutekeleza mapenzi yake.

Bikira Maria ni kielelezo halisi cha neema; Israeli mpya anayesimuliwa na Maandiko Matakatifu kama mchumba; picha ambayo inaelezea pia upendo wa Kristo kwa Kanisa lake; analisafisha na kulitakasa ili liweze kuwa ni takatifu liking'ara kwa utukufu pasi na mawaa! Hii ndiyo picha ambayo Mababa wa Kanisa katika kuelezea Mafundisho Tanzu ya Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili. Kanisa ni Bikira na Mama, kama alivyo Bikira Maria ambaye amebahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria anawasaidia waamini kufahamu maana ya dhambi ya asili, kwani ndani mwake, kuna uhusiano wa dhati kati yake na Mwenyezi Mungu; uhusiano ambao mara nyingi unavurugwa na dhambi; ndani ya Bikira Maria umoja na maelewano pasi na kujibakiza. Bikira Maria amekingiwa dhambi na kwa jinsi hii ni mali ya Mwenyezi Mungu na amejaa neema na upendo wake.

Mafundisho Tanzu kuhusu Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni kielelezo cha imani hai ambamo ahadi za Mwenyezi Mungu zimepata utimilifu wake; Agano lake ni mzizi ambamo kumezaliwa Tunda lililobarikiwa duniani, Yesu, Mkombozi. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni kielelezo cha neema inayotoa jibu kwamba, uaminifu kwa Mungu unazaa imani ya kweli na thabiti.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewaambia waamini, mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwamba, jioni alikuwa anatarajia kwenda kwenye Uwanja wa Spagna kwa ajili ya kutoa heshima zake kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Bikira Maria Mama wa Mungu ni mfano wa kuigwa, kwani hata ndani ya waamini neema ya Bwana inaweza kupata jibu la imani ya kweli na inayoweza kuzaa matunda.







All the contents on this site are copyrighted ©.