2012-12-07 14:41:22

Mafundisho Jamii ya Kanisa na Mafundisho Tanzu ya Imani ni chemchemi inayopania kumwilisha Amri ya Upendo kwa Mungu na Jirani


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa, tarehe 7 Desemba, 2012 amewashukuru wajumbe wa Tume ya Kitaalimungu Kimataifa kwa mchango wao unaopania kutumia vyema akili kwa ajili ya imani na furaha ya waamini, kama inavyojionesha katika Ujumbe wao kwa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Hii inaonesha mwanga ambao wanataalimungu wanapohudumia kwa uaminifu mkubwa ukweli wa kiimani wanaweza kushiriki pia katika mwamko wa Uinjilishaji Mpya unaovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa sasa. Ujumbe huu anasema Baba Mtakatifu unabainisha hali ya wanataalimungu kwa nyakati hizi: matarajio, kanuni na vigezo wanavyopaswa kutumia mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yanayotoa utambulisho makini katika umoja na utofauti katika utekelezaji wake.

Nyaraka hizi zinabainisha jinsi ambavyo Taalimungu inavyoweza kuwa ya Kikatoliki na yenye uwezo wa kuchangia katika utume wa Kanisa wa kutangaza Injili ya Kristo kwa watu wote. Kuna sehemu za kitamaduni ambazo Taalimungu haipewei msukumo wa pekee katika ulimwengu wa wasomi kutokana na uhusiano wake na Imani jambo ambalo linaweza kuleta uelewa potofu kwa kudhani kwamba, Taalimungu ni sehemu ya sayansi za kidini.

Tume hii inakumbusha kwamba, Taalimungu inajikita katika Imani na Akili na kwamba, uwepo wa somo hili katika taasisi na vyuo vikuu linapata mwono mpana na kamilifu wa akili ya mwanadamu. Wanataalimungu wanapaswa kuwa waaminifu kwa kweli za kiimani anasema Baba Mtakatifu, kwani jambo hili ni muhimu sana katika imani na maisha ya Kanisa.

Watu wa Mungu wanasema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwamba, wanashiriki Unabii wa Kristo waliojitwalia kwa kumpokea Roho Mtakatifu, kumbe hawapaswi kukosea kuamini na kuonesha kipaumbele chake katika Imani ya Watu wa Mungu. Hisia ya Imani, "Sensum Fidei" ni kipimo kinachomwezesha mwamini kutambua ikiwa kama ukweli unaotangazwa unapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa; ni mwono unaomwezesha mwamini pia kupata ukweli mtimilifu. Ni vyema watu kuwa na vigezo vitakavyowawezesha kupambanua hisia za kiimani ambazo ni kweli na zisizo za kweli.

Baba Mtakatifu anasema, Hisia ya Kiimani inapata ukamilifu wake pale tu mwamini anaposhiriki kikamilifu katika maisha ya Kanisa pamoja na kuwajibika kwa viongozi wake. Mwelekeo huu wakati mwingine, umepelekea matumizi ya nguvu kwa madai kwamba wanatangaza ukweli kwa wote. Baadhi ya watu wanachagua tunu msingi ambazo zinaweza kusaidia kujenga utamaduni wa kuvumiliana na amani kama kielelezo cha Jamii inayojengeka katika misingi ya demokrasia pana zaidi.

Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu, ni kiini cha umoja miongoni mwa watu; Ukristo na Imani kwa Mungu mmoja, ni mada ambayo ni hai kabisa na inagusa ukweli wa maisha ya mwanadamu nyakati hizi. Imani kwa Mungu mmoja, Muumba wa mbingu na dunia inahitaji akili na tafakari ya kina, mambo yanayopaswa kuimarisha Ufunuo wa Fumbo la Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu; Fumbo ambalo linapata utimilifu wake kwa Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, alikataa aina zote za chuki na matumizi ya nguvu, akakumbatia upendo na kwamba, kinzani na misigano ya kidini inapata chimbuko lake katika historia ya mwanadamu, kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu. Watu wanapofanya rejea katika kweli na haki, wanafungua mlango wa majadiliano unaoratibu mahusiano ya watu ndani ya Jamii husika.

Maana halisi ya maisha na kanuni maadili ni mambo yanayomwezesha mtu kutenda kwa haki na kusimama kidete kulinda na kutetea amani. Mwanadamu akimweka Mungu kuwa ni kiini cha maisha yake anaweza kuanza hija ya upatanisho wa kweli iliyoanzishwa kwa njia ya Msalaba wa Yesu, amani ya watu wake na msingi wa umoja na udugu. Mafundisho Jamii ya Kanisa na Mafundisho Tanzu ya Imani ni chemchemi ya Imani inayopania kumwilisha Amri ya Upendo katika hali mbali mbali za maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.