Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni kielelezo makini cha Imani, Matumaini na
Mapendo
Mheshimiwa Sr. Palma Porro, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Bikingira Maria Mkingiwa
Dhambi ya Asili la Ivrea anasema, Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa
Dhambi ya Asili ni wakati wa kufanya tafakari ya kina na kumwimbia Mwenyezi Mungu
utenzi wa sifa na shukrani.
Karama ya Shirika inawachangamotisha Masista kujitoa
bila ya kujibakiza kwa kumuiga Bikira Maria, kielelezo makini cha imani na matumaini
kwa Mwenyezi Mungu.
Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili ni kielelezo muhimu
cha ubinadamu uliokombolewa kutokana na dhambi na mauti, changamoto ya kujitoa kwa
ajili ya kutangaza Injili ya Upendo na Matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Ni Mama ambaye
alifahamu shida na mahangaiko ya watu wa nyakati zake; akashuhudia kwa mshangao mkubwa,
Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo akiteswa na kufa Msalabani, lakini bado akaendelea kubaki
na imani thabiti juu ya Mwana wa Mungu, akabahatika kushiriki katika Mpango wa Kazi
ya Ukombozi kama wanavyobainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Ni
Mama aliyekubali mpango wa Mungu tangu wakati ule alipohabarishwa kuhusu kuzaliwa
kwa Masiha hadi pale aliposimama chini ya Msalaba, mwaliko kwa waamii kujitoa bila
ya kujibakiza katika huduma inayojionesha kwa namna ya pekee katika hija ya maisha
ya imani, utii, upendo na matumaini.
Hata leo hii anasema Mheshimiwa Sr Palma
kwamba, inawezekana kabisa mtu kujitoa bila ya kujibakiza katika raha na shida kwa
kujichotea nguvu na neema inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni
mwaliko kwa kila mwamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kujitahidi kuwa huru
pasi na mawaa ya dhambi.
Ni mwaliko wa kuendelea kufanya hija kutoka katika
ubinafsi na usalama na hivyo kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu anayeonesha njia
ya kupata uhuru kamili, utambulisho wa kibinadamu, furaha ya kweli inayobubujika kutoka
katika undani wa mt una amani ya kweli. Imani inamchangamotisha mwamini kujiachilia
mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa kuonesha uhuru kamili kama alivyofanya Bikira Maria.
Ni kielelezo cha imani na fadhila zilizokomaa na hatimaye, kumwilishwa kwa
njia ya huduma ya upendo kwa jirani. Ni Mama aliyeonesha fadhila zote hizi katika
uhalisia wa maisha yake. Ni mwanamke aliyekuwa na ukarimu wa ajabu, akaonesha uwepo
wake wakati alipohitajika. Alikuwa na upendo mkamilifu, akasamehe na kusahau akiwa
na moyo wazi kabisa!
Bikira Maria ni kielelezo cha imani thabiti na majitoleo
yanayoonesha njia ya kuweza kukutana na Yesu Kristo na hivyo kuanza kufuata nyayo
zake na kuonesha ubinadamu mkamilifu; mwanga wa matumaini thabiti na imani kwa maisha
yao kwa sasa kwa siku za usoni.
Mheshimiwa Sr. Palma Porro anaikumbusha Familia
ya Waverniani kwamba, uaminifu kwa wito wao, unapata chimbuko lake katika imani na
hali ya kujitoa bila ya kujibakiza. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni Mama
aliyefanya hija ya imani awasindikize watoto wake katika uhuru wa kweli, ili waweze
kuwa ni kielelezo na mfano wa Watoto wa Mungu, Watakatifu na wasio na mawaa katika
upendo.