2012-12-07 08:11:28

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa na ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Kitaifa inayoadhimishwa nchini Italia kila mwaka ifikapo tarehe 5 Desemba, wanasema kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaendelea kuonesha makucha yake kwa mamillioni ya watu kiasi kwamba, watu wengi wanajiona kwamba, hawana thamani tena, hawaoni maana ya kuishi na kwamba, matumaini yao yanaendelea kugonga mwamba.

Hali mbaya ya uchumi inawafanya watu wengi kujitumbukiza katika mambo ambayo ni hatari kwa maisha na afya yao! Wanatafuta majibu ya mkato kwa njia ya ulevi wa kupindukia, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Ni watu ambao wameelemewa na mchezo wa kamali, kiasi kwamba, wanaendelea kupoteza hata kile kidogo walicho nacho!

Ni watu wanaodhani kwamba, kwa njia ya maisha duni kama haya wanaweza kupata suluhu ya shida na mahangaiko yao ya ndani, lakini kwa bahati mbaya, hii ni suluhu ya muda mfupi inayosababisha madhara makubwa katika afya ya akili. Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, wagonjwa wa afya ya akili wanaendelea kuongezeka maradufu.

Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, kwa kutambua shida na mahangaiko ya watu mbali mbali ndani ya Jamii, daima linatamani kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwatangazia watu kwamba, Mungu ni Upendo. Ndiyo maana Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Italia, kuhakikisha kwamba, wanaitumia Jumapili ya kwanza ya Mwezi Desemba kwa ajili ya kufanya tafakari ya kina kuhusu wagonjwa wa afya ya akili pamoja na familia zao; ambao mara nyingi wanajikuta kana kwamba, wametengwa na kusahauliwa na Jamii husika.

Wahudumu wa afya ya akili wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa kuzingatia na kuheshimu utu wa kila mtu hata wagonjwa hawa katika mahangaiko yao ya ndani. Jamii ijitahidi kujenga uhusiano mwema na wagonjwa pamoja na familia zao, kama kielelezo cha matumaini na mshikamano wa kidugu hasa katika shida na mahangaiko. Washirikishwe pale inapowezekana katika maisha ya Kijamii. Kila mtu awajibike kujenga na kuimarisha fadhila ya Matumaini.

Jumuiya za Kikristo ziwe wazi kuwapokea na kuwamegea watu hawa kwa kuwaonjesha wema na ukarimu wa Mama Kanisa anayetibu na kufariji; Kanisa liwe ni ni mahali pa maboresho ya afya pamoja na Matumaini. Kwa njia hii, Familia ya Mungu inayowajibika, italiwezesha Kanisa kutekeleza wajibu na dhamana yake kwa kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na afya pamoja na matatizo mengine waliyo nayo. Siku ya Afya ya Akili Kitaifa, iwe ni fursa ya kuonesha moyo wa upendo na mshikamano endelevu.









All the contents on this site are copyrighted ©.