2012-12-05 09:13:57

Viongozi Barani Afrika dumisheni misingi ya utawala bora, haki, amani na upatanisho


Askofu mkuu mstaafu Desmond Tutu wa Jimbo kuu la Cape Town, Afrika ya Kusini, anawahimiza wananchi wa Kenya kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini Kenya hapo tarehe 4 Machi 2013 unakuwa huru na haki; kwa kuzingatia kanuni na sheria za Nchi, ili amani iweze kutawala.

Watu wengi Barani Afrika anasema Askofu mkuu Tutu kwamba, wana matumaini makubwa na wananchi wa Kenya katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na demokrasia. Sala zinazotolewa na waamini wa Makanisa na Dini mbali mbali nchini Kenya, hazina budi kwenda sanjari na vitendo pamoja na dhamiri nyofu, inayopania kuhakikisha kwamba, uchaguzi unatawaliwa na misingi ya haki, amani na ukweli.

Askofu mkuu Tutu alikuwa anatoa mada kwenye Kongamano la Kimataifa la Makanisa Barani Afrika, uliofunguliwa hapo tarehe 4 Desemba na unatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 6 Desemba 2012. Tema inayoongoza mkutano huu ni "Kanisa Barani Afrika; fursa, changamoto na nyajibu". Huu ni mkutano unaohudhuriwa na wajumbe mia moja na sitini kutoka katika Makanisa mbali mbali Barani Afrika.

Askofu mkuu Tutu anawaalika viongozi wa Serikali Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanadumisha misingi haki, amani na upatanisho wa kweli sanjari na kuondokana na vitendo vinavyosababisha rushwa, ufisadi naubinafsi; mambo ambayo yamepekea kuyumba kwa misingi ya uongozi bora Barani Afrika. Ni wajibu na dhamana ya viongozi Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanajenga mazingira bora zaidi, ili kurudisha sifa na heshima kwa Bara la Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.