Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu ni Jukwaa makini la Uinjilishaji!
Askofu Martin Kivuva wa Jimbo Katoliki Machakosi, Kenya, hivi karibuni alikutana na
Wanachuo kutoka Chuo Kikuu cha Daystar waliomtembelea nyumbani kwake, ili kujifunza
kuhusiana na masuala mbali mbali ya kichungaji. Askofu Kivuva amekazia umuhimu wa
Kanisa kuendeleza shughuli za kichungaji miongoni mwa wanafunzi wa taasisi za elimu
ya juu na vyuo vikuu, kwani hili ni jukwaa muhimu sana la Uinjilishaji ndani ya Kanisa.
Mapadre
na Watawa wanaosoma kwenye taasisi na vyuo vikuu, wanapaswa pia kutambua dhamana na
wajibu wao wa kuendelea Kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha na kamwe wasiwakatishe
tamaa vijana wengine kutokana na maisha yao ambayo pengine hayamtangazi Kristo kwa
umakini mkubwa. Masomo na Uinjilishaji vyuoni ni mambo yanayoweza kwenda pamoja.
Wanafunzi
wa taasisi za elimu na vyuo vikuu, sehemu kubwa wanakabiliwa na changamoto ya kumong'onyoka
kwa misingi bora ya maadili na utu wema; kupenda mno malimwengu; matumizi haramu ya
dawa za kulevya, ukahaba pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali fedha wanayopewa
wakati wakiwa masomoni. Hizi ni dalili ambazo zinaonesha haja kwa Mama Kanisa kujipanga
vyema zaidi, ili kuwasaidia wanavyuo kutambua na kuthamini uwepo wao vyuoni kama mahali
pa kujipatia elimu, ujuzi na maarifa pamoja na kuimaarisha imani yao, kwa njia ya
ushuhuda amini wa maisha.