Katika kitogoji cha Isiro, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo linalojulikana
kwa myumba wa kisiasa, vurugu na mateso hasa kwa wanawake, hapo tarehe 1 Desemba
1964, alifariki Sista Marie Clementine Anuarite.
Mtawa huyu wa Usharika
wa Masista wa Familia Takatifu ya Wamba, alitangazwa kuwa Mwenye Heri na Papa Yohane
Paulo II tarehe 15 Agosti 1985, wakati wa ziara yake ya kichungaji Kinshasa, mji mkuu
wa DRC.
Katika Mwaka huu wa Imani na shuhuda thabiti hata kama ni kukikabili
kifo, na wakati huohuo kuwa tayari kusamehe watesi, kabla ya kutoa pumzi ya mwisho,
Mwenye Heri Anuarite, bikira na shahidi, anakuwa mfano wa kufuata hasa katika mataifa
ya Afrika, katika mtazamo na azma ya kuheshimu utu wa mtu , maridhiano na amani,
kwa watu wote wenye mapenzi mema.
Mandhari hii ilihamasishwa katika Kipindi
Jumamosi cha Afrofonia, Desemba 1, 2012, ambayo ni Siku Kuu ya Kilitulujia ya Mwenye
Heri Anuarita. Kipindi kiliwasilishwa na Maria Josè Muando Buabualo wa Idhaa ya
Kifaransa na pia mchango kutoka kwa Dulce Maria Araujo Évora, wa Idhaa ya Kireno
wote wa Redio Vatican kwa Afrika, na Augustin Bita, mchungaji wa jumuiya ya Wakatoliki
wanaotoka Kongo, ambao kwa sasa wanaishi hapa Roma. Nyote mwaalikwa kusikiliza.