2012-12-05 07:59:29

Kanisa Barani Amerika linakusanyika Mjini Vatican kwa Kongamano litakalopembua kuhusu: Mwaka wa Imani, Uinjilishaji Mpya na Changamoto zilizopo!


Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini, Jumanne tarehe 4 Desemba 2012 ameongoza jopo la viongozi waandamizi kutoka Vatican, ili kuelezea juu ya Kongamano la Kimataifa litakalofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 9 hadi 12 Desemba 2012 ili kuzungumzia hali ya Kanisa Barani Amerika katika kipindi cha miaka kumi na mitano iliyopita, baada ya maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Kanisa la Amerika ya Kusini, iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako mwaka 1997.

Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu "Kukutana na Yesu Kristo aliye hai: njia ya wongofu, umoja na mshikamano Barani Amerika." Katika kipindi cha miaka kumi na mitano iliyopita, Kanisa nchini Marekani, Canada na Amerika ya Kusini, limeendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake. Tema ya wahamiaji imeendelea kuwa tete katika majadiliano na wanasiasa; mtandao wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na sera zinazotumika kudhibiti biashara hii ni kati ya mada tete zitakazojadiliwa na wajumbe kwenye Kongamano hili.

Kardinali Marc Ouellet anasema kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya jinai, kinzani, migogoro, vurugu na fujo zinazofanywa na kundi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira. Taasisi ya Familia imeendelea kukabiliana na kinzani pamoja na utamaduni wa kifo unaotishia Injili ya Uhai; uhuru wa kidini, umaskini na hali ya kukata tamaa ni kati ya mambo yanayohatarisha misingi ya haki, amani na utulivu.

Wajumbe wanatarajiwa kujadili matatizo na changamoto zote hizi katika mwanga wa Utume wa Kanisa, ili kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano baina ya Makanisa mahalia, wakitambua kwamba, kwa pamoja wanaunda Kanisa la Kiulimwengu. Ndiyo maana Kongamano hili linafanyika mjini Vatican, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, mchungaji mkuu.

Professa Guzman Carriquiry Lecour anasema kwamba, jumla ya wajumbe mia mbili wanatarajiwa kushiriki katika Kongamano hili. Baadhi yao ni kutoka kwenye Mabaraza ya Kipapa, Makardinali, Maaskofu wakuu, wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na wawakilishi wa waamini walei. Ni kongamano ambalo litawahusisha Mabalozi mbali mbali kutoka katika Barani Amerika.

Jumapili tarehe 9 Desemba, 2012 Wajumbe wa Kongamano watafungua kwa Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican na baadaye Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, atawasalimia na kuwapatia ujumbe wake wa kitume, chachu ya kufanyia kazi wakati wa Kongamano hili.

Kongamano hili litafungwa pia kwa Ibada ya Misa Takatifu, tarehe 12 Desemba 2012, Kanisa litakapokuwa linafanya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika. Ni Ibada itakayowashirikisha waamini wengi kutoka Amerika. Juhudi zote hizi ni katika mwendelezo wa mchakato wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani na juhudi za Uinjilishaji Mpya; dhamana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Dr. Carl Anderson, Kiongozi mkuu wa Knights of Columbus, anakazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Uinjilishaji Barani Amerika; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ari na uchangamfu mkubwa zaidi, jukumu ambalo waamini walei wanapaswa kulivalia njuga, kwa kushirikiana na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na utamadunisho, kwa kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inaota mizizi katika maisha na vipaumbele vya waamini. Bikira Maria wa Guadalupe, awasaidie waamini kumwendea Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.