Iweni mashahidi wa Kristo kwa njia ya: Imani. Mapendo na Matumaini
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe
5 Desemba 2012 katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ametafakari kuhusu Kipindi cha
Majilio, kinachowakirimia waamini fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu ukuu wa
Mungu katika Mpango wa Ukombozi. Utenzi unaofungua Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Waefeso,
unamshukuru Mwenyezi Mungu kwa huruma na mapendo yake makuu aliyewachagua katika Kristo
kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu ili kuwafanya kuwa ni watoto wake.
Baba
Mtakatifu anasema, Mpango wa Mungu ni kuvijumuisha vitu vyote katika Kristo. Mwenyezi
Mungu ameufunua Mpango wake kwa njia ya Ufunuo unaopata hitimisho lake katika Fumbo
la Umwilisho wa Mwana wa Mungu na kwa njia ya ujio wa Roho Mtakatifu. Kujifunua kwa
Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo ni kuna endana na matumaini pamoja na matamanio
ya binadamu; mwaliko kwa waamini kuweza kuitikia kwa kuonesha utii wa Imani kwa Mwenyezi
Mungu.
Kitendo cha mwamini kuinua akili na utashi wake kwenye ufunuo wa Kimungu;
ni mwaliko wa kiimani kutubu na kuanza kuona ukweli wa maisha na ulimwengu unaowazunguka
kwa mtazamo mpya. Kipindi hiki cha Majilio, ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina
kuhusu uzuri wa Upendo wa Mungu katika kazi ya Ukombozi sanjari na kujitahidi kuwa
ni alama hai ya uwepo wake ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na
watu wote wenye mapenzi mema kwa njia ya upendo, imani na matumaini wanaweza kuwa
ni mashahidi wa uwepo wa Mungu duniani.
Amewashukuru kwa namna ya pekee, mahujaji
waliofika mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya kutangazwa kwa Mtumishi wa Mungu
Sista Maria Crescenzia Perez kuwa Mwenyeheri, changamoto na mwaliko kwa kufuata nyayo
zake kwa uaminifu na furaha, huku wakijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza
Injili. Amelishukuru Shirikisho la Waoka Mikate Italia kwa zawadi ya mikate waliyompatia
kwa ajili ya huduma ya upendo wa Papa.