Washeni moto wa mapendo kwa Kristo, Kanisa, Adhimisho la Ekaristi Takatifu ili kuzima
kiu na njaa ya watu wenu!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu, tarehe 3 Desemba 2012 amekutana
na Jumuiya cha Chuo Kikuu cha Mwenyeheri Beda, kilichoko mjini Roma, maalum kwa ajili
ya wanafunzi wanaotoka Uingereza. Anasema, anaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili
Chuo hiki kiendelee kuwa ni kitalu cha miito mitakatifu kwa ajili ya Upadre na Maisha
ya Kitawa.
Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa Katoliki nchini Uingereza ambalo
limetoa Wamissionari wengi kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo sehemu mbali mbali
za dunia, kama ilivyokuwa kwa Papa Gregori mkuu aliyemtuma Mtakatifu Augustine wa
Cantebury kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini Uingereza. Matokeo ya kazi hii kubwa
yanajionesha kwa namna ya pekee katika kipindi cha miaka mia sita na hamsini ya Imani
na Ushuhuda uliooneshwa na waamini mbali mbali nchini humo.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini nchini Uingereza kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwasha moto wa
imani kwa bidii na umakini mkubwa, ili Kristo aendelee kufahamika zaidi na zaidi,
kwa njia ya ushuhuda wa yale ambayo wameyasikia kutoka kwa Mitume.
Watakatifu
mbali mbali wameendelea kuwaonesha waamini upendo wenye mvuto unaowaelekeza wengine
kwa Kristo ili waweze kumfahamu zaidi, huo ukawa ni mwanzo wa kuenea Habari Njema
Uingereza, Canada na katika nchi za Scandinavia.
Kuna watu waliomwaga damu
yao kwa ajili ya Kristo, ili aweze kufahamika na kupendwa, changamoto kwa Wanajumuiya
hii kusali daima, kujenga utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Kusikiliza
kwa makini Neno la Mungu; daima wakiwa tayari kutolea ushuhuda wa Imani yao kama walivyokuwa
wafuasi wa Kristo, kwa njia ya maisha na utume wa Kipadre, kwa ajili ya wokovu wa
ulimwengu. Yesu amewachagua kama marafiki zake, changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza
katika utekelezaji wa kazi ya Ukombozi sanjari na Uinjilishaji Mpya.
Baba Mtakatifu
anawaalika Wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Mwenyeheri Beda kuwasha ndimi za moto zinazoleta
mabadiliko katika maisha ya watu, kama inavyojionesha kwenye Agano la Kale na pale
Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume siku ile ya Pentekoste. Mwanga huu uwe ni nguvu
ya upendo wa Mungu unaosafisha Jumuiya au Taifa husika.
Moto huo uwashe mapendo
kwa Kristo, Kanisa na Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuzima kiu na njaa ya maisha
ya kiroho kwa kutambua kwamba, wanaweza kushibishwa kwa kumfahamu, kumpenda na kumtumikia
Kristo. Ni mwaliko wa kuwatangazia ukweli wa Kiinjili kwa njia ya mapendo; wakiwaonesha
Kristo ambaye ni Mkate wa Uzima wa milele. Mwanga wa Kristo uoneshe utakatifu wa maisha
yao, kwa kuendelea kufuata nyayo za watakatifu kutoka Uingereza waliotolea ushuhuda
wa upendo wa Mungu kwa gharama ya maisha yao; mwaliko kwa kila mmoja wao pia kutamani
utakatifu.