2012-12-03 08:20:03

Toba na wongofu wa ndani ni njia ya kujenga mshikamano wa kitaifa unaojikita katika upatanisho, haki na amani


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni limehitimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, kwa mwaliko kwa Familia ya Mungu nchini humo kwanza kabisa kutubu na kuongoka pamoja na kuomba msamaha wa dhambi zilizotendwa wakati wa machafuko ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, yapata miaka arobaini na mbili iliyopita, pamoja na kinzani na migogoro mingine inayoendelea kufuka moshi nchini humo.

Haya ni matukio wanasema Maaskofu ambayo yamepelekea maelfu ya watu kupoteza maisha yao pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu; mambo ambayo kimsingi yanarudisha maendeleo ya watu nyuma: kiroho na kimwili, kiasi hata cha kutishia amani na utulivu wa wananchi wa Nigeria kwa sasa.

Askofu mkuu Ignatius Kaigama katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee haja ya toba, wongofu, msamaha pamoja na upatanisho, kama njia ya kuweza kupata amani ya kudumu nchini Nigeria. Hii ndiyo changamoto ambayo ilitolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, wakati wa Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka elfu mbili ya Ukristo, kwa kuomba radhi hadharani kutokana na makosa yaliyotendwa na Watoto wa Kanisa, hata kama anatambua kwamba, Kanisa ni Takatifu kwani muasisi wake ni Yesu Kristo, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Nigeria, liliwajumuisha wajumbe elfu tatu kutoka sehemu mbali mbali za Nigeria, wakiongozwa na kauli mbiu “Umoja wa Kitaifa kwa njia ya upatanisho, haki na amani. Maaskofu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu waliwaalika waamini kuchunguza dhamiri zao na kufanya toba ya kweli kutokana na machafuko yaliyosababishwa na kinzani za kikabila, zilizopelekea vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Nigeria, iliyomaliza kunako mwaka 1971.

Tangu wakati huo, cheche za kinzani, chuki na uhasama zimeendelea kukua na kuongezeka siku hadi siku, na matokeo yake ni chuki na uhasama ambao sasa unachuku sura ya kidini.

Wananchi wa Nigeria wanapaswa kujibidisha kutafuta uponywaji wa ndani, ili kuanza hija mpya ya maisha inayojisimika katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kinzani na migogoro ya kidini, kikabila, kisiasa na kijamii haina tija wala maendeleo kwa wananchi wa Nigeria wanasema Maaskofu.

Umefika wakati wa kutupilia mbali yaliyopita kwa njia ya toba na msamaha wa kweli, ili kujenga na kuendelea kuimarisha upendo na amani, fadhila zinazoondoa cheche za chuki na uhasama kati ya watu.








All the contents on this site are copyrighted ©.