Majaalim wabainisha changamoto wanazokabiliana nazo katika sekta ya elimu ya juu
Professa Paolo Paris, Mkuu wa Chuo Kikuu cha “Foro Italico”, akizungumza
kwa niaba ya walezi wenzake kutoka katika taasisi na vyuo vikuu vilivyoko mjini Roma,
wakati wa Masifu ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican, Jumamosi tarehe Mosi Desemba, 2012 anasema kwamba, kwa sasa wanakabiliana
na kinzani zinazohatarisha urithi, mfumo, maudhui pamoja na malengo ya majiundo kwenye
vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Kuna wakati vyuo vikuu lilikuwa ni
jukwaa la majiundo makini, mahali pa upembuzi yakinifu pamoja na kurithisha ujuzi
na maarifa. Ilikuwa ni fursa ya kukua na kukomaa kitamaduni na kimaadili; lakini leo
hii, misingi hii iko hatarini kwani inapimwa na mizani ya maendeleo, fursa za ajira,
usawa, mshikamano, uhusiano wa dhamiri ya mtu na sheria maadili pamoja na mambo kadhaa
yanayowazunguka wakati mwingine yakiwa na mwelekeo hasi zaidi.
Vyuo vikuu vinachangamotishwa
kutambua na kuthamini uwepo wa Mwenyezi Mungu na kwamba, mwanadamu ana kiu ya kutaka
kuonana naye. Kongamano la Majaalim Kimataifa, litakuwa na wajibu wa kubainisha umuhimu
wa tamaduni mbele ya Mweyezi Mungu. Huu utakuwa ni mchango makini wakati wa maadhimisho
ya Mwaka wa Imani.
Professa Paris anasema, ulimwengu mamboleo umegubikwa mno
na ubinafsi, madhara yake wakati mwingine yanajionesha hata katika Kanisa, ambalo
vijana wanaliona kuwa ni kielelezo cha matumaini. Hili ni Kanisa katika mchakato wa
Uinjilishaji Mpya linaloalikwa kuunda watu wenye utu mpya unaowawajibisha kijamii,
kwa kutoa majibu makini yanayopata chimbuko lake katika maisha ya kiroho, kiutu na
kimaadili mintarafu utendaji wa shughuli za kijamii.
Huu ni mwaliko wa kuendeleza
majadiliano, kwa kutafuta zaidi, kile kinachowaunganisha ili kuvuka vikwazo na kinzani
zisizo na tija, kwa ajili ya maisha ya mwanadamu. Walezi hao wametumia fursa hii kumtakia
matashi mema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika kipindi hiki cha Majilio
na hatimaye, wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2012.