2012-12-03 08:24:50

Changamkieni mikakati ya Uinjilishaji Mpya kama sehemu ya mwendelezo wa Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Enugu


Askofu mkuu Augustine Kasujja Balozi wa Vatican nchini Nigeria, katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki la Enugu, hivi karibuni, amewataka waamini kujikita zaidi katika kupanga na kutekeleza mikakati inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya, kama changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Enugu yanakwenda sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto ya kusoma alama za nyakati kama walivyobainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kipindi cha shukrani kwa Wamissionari na Waamini wa kwanza kwanza waliojitosa kimaso maso kupokea Injili ya Kristo na kuendelea kuikumbatia kama dira katika maisha yao kwa kipindi cha miaka hamsini iliyopita.

Jimbo la Enugu, Nigeria, limekuwa na mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa ni mahali ambapo kuna Seminari kuu ya Kanda, ambayo imekuwa ni kitalu cha majiundo ya Kipadre nchini Nigeria na matunda yake yanaendelea kuonekana sehemu mbali mbali za dunia. Huduma za Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ni kati ya mchango mkubwa wa Jimbo Katoliki la Enugu kwa wananchi wa Nigeria.

Askofu mkuu Augustine Kasujja anaialika Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Enugu, Nigeria, inapofungua ukurasa mpya baada ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo hilo, kujikita zaidi na zaidi katika Utangazaji wa Neno la Mungu sanjari na Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa maisha amini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.