2012-12-03 08:15:11

Baba Mtakatifu Benedikto XVI na matumizi ya Mitandao ya Jamii


Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anasema kwamba, Kanisa limeendelea kusoma alama za nyakati kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu, jambo ambalo hata Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anaendelea kulivalia njuga, ili kwa njia ya mitandao ya jamii inayoendelea kukua na kupanuka, aweze kujenga jukwaa la mawasiliano na umati huu mkubwa.

Habari za Baba Mtakatifu kuanza kutumia mtandao wa kijamii unaojulikana kama Twitter ni habari ambayo imeenea kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia. Lakini ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu tangu Juni 2011 alizindua Mtandao wa Vatican: kwa kutumia Twitter.

Hii ni changamoto chanya kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anayelitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linatumia kwa ukamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwani hii ndiyo njia rahisi zaidi ya kuweza kuwafikia watu wengi zaidi, ikilinganishwa na njia nyingine ambazo zimekuwa zinatumiwa na Mama Kanisa, tangu kuanzishwa kwake.

Baba Mtakatifu ameendelea pia kuwasiliana na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya mtandao @Pope2YouVatican. Ni mtandao unaowawezesha vijana kuwasiliana na Baba Mtakatifu kwa njia ya mitandao ya kijamii, kama ilivyo pia kwenye Youtube na Facebook. Lengo kuu ni kuzungumza na watu wanaoishi katika ulimwengu wa utandawazi kwa njia za kisasa. Anataka kutangaza Imani kwa wale wanaotumia mitandao ya jamii, ili pia waweze kuonja utajiri wa Imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; Imani inayoleta mabadiliko na kumwonjesha mwanadamu matumaini katika hali zake mbali mbali.

Baba Mtakatifu anataka kuwasiliana na vijana wa kizazi kipya katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu wala mbwembwe! Bali ni kuwavuta wengi zaidi waweze kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu mingi wa rehema na neema; upendo na msamaha wa kweli. Mitandao ya Jamii itatumiwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuonesha mawazo yake makuu wakati wa hotuba, mahubiri au ujumbe wake kwa matukio mbali mbali.

Baba Mtakatifu anaanza matumizi ya mitandao ya jamii kwa tafakari zake za kila Jumapili wakati wa Sala ya Mchana., kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.