UNICEF yasema, maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto
yamepungua, lakini lengo bado halijafikiwa!
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF linabainisha kwamba, maambukizi
ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto yamepungua, lakini lengo kuu
la UNICEF ni kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na kizazi kisichokuwa na
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Lengo hili linaweza kutimia ikiwa kama wanawake wajawazito
na watoto walioathirika kwa Virusi vya Ukimwi watapata matibabu muafaka.
Takwimu
zinaonesha kuwa, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto
wakati wa kujifungua yamepungua kwa asilimia ishirini na nne katika nchi ishirini
na mbili na nyingi kati ya hizi ni zile ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara. Jumuiya
ya Kimataifa anasema Bwana Anthony Lake, haina budi kuhakikisha kwamba, inatoa dawa
kwa watu wazima, ili kusaidia kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani.
Watoto wapimwe na kupewa huduma stahiki kadiri ya mikakati ya Umoja wa Mataifa.
Huduma
ya afya kwa wanawake wajawazito wenye Virusi vya Ukimwi, itawawezesha wanawake hawa
kuishi kwa muda mrefu zaidi pamoja na kutoa hifadhi kwa watoto wao, ili wasiambukizwe
na Virusi vya Ukimwi. Lengo liwe ni kuhakikisha kuwa, hakuna tena maambukizi mapya
ya Virusi vya Ukimwi, ifikapo mwaka 2015.