2012-12-01 08:32:26

Siku ya Kupambana na Ukimwi Duniani, 1 Desemba 2012


Malengo ya Maendeleo ya Millenia kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2015 yanapania kuhakikisha kwamba maambukizi ya ugonjwa huu yanapungua maradufu. Hadi sasa kuna dalili za mafanikio kutokana na jitihada zinazofanywa na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Takwimu za Umoja wa Matifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kumekuwepo na ongezeko kubwa la udhibiti na huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi sehemu mbali mbali za dunia, mafanikio ambayo yamewezesha walau kurefusha maisha ya wagonjwa wa Ukimwi.

Jambo la msingi kwa sasa anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Kimataifa, inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe Mosi, Desemba, kwamba, kuna haja ya kuendeleza juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto sanjari na kuwawezesha wanawake wajawazito wanapata dawa za kurefusha maisha.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, anazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuondoa tabia ya unyanyapaa kwa wagonjwa wa Ukimwi, hali ambayo inaendelea kugumisha maisha ya watu wenye maambukizi ya Ukimwi. Kuna sheria na sera potofu ambazo zinajikita katika hofu na mashaka bila kuzingatia ukweli wa kisayansi zinazopelekea ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Kuna haja kwa Jamii kupata habari zenye uhakika kuhusu UKIMWI, kupima na kupata matibabu kwa magonjwa nyemelezi, kama sehemu ya utekelezaji wa haki msingi kwa tiba, jambo ambalo ni sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya Ukimwi. Kila mtu akitekeleza wajibu na dhamana yake, kuna uwezekano mkubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na kizazi ambacho hakuna virusi vya Ukimwi, ifikapo mwaka 2015. Kila mdau ajifunge kibwebwe kuhakikisha kuwa anaendeleza mafanikio yaliyokwisha kupatikana hadi sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.