2012-12-01 14:58:07

Kipindi cha Majilio ni mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa ndani


Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, Italia, katika kipindi cha Majilio anawaalika waamini kujitaabisha kuutafuta ili hatimaye, kuuona wokovu unaoletwa na Masiha, kwani kila mtu atauona. Ni ufalme unaojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa Watu wa Mataifa.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wokovu ni kwa watu wote, kwani hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopata utimilifu wake kwa njia ya Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia. Kwa njia ya Kanisa, wote wanapata fursa ya kufanyika Watoto wa Mungu na hivyo wanatumwa kwenda duniani kote kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwani Ukristo ni dini ya watu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, kama ambavyo aliwahi kusema, Baba Mtakatifu Paulo wa sita.

Kiini cha Habari Njema ya Wokovu ni Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, atarudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ili kufanikiwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani. Hii ndiyo njia iliyooneshwa na Yohane Mbatizaji wakati alipokuwa anahubiri kuhusu Ubatizo wa Toba kwa maondoleo ya dhambi, jambo ambalo linakamilika hatua kwa hatua. Toba na mwongofu wa ndani ni mambo yanayomwezesha mwamini kubadili mtindo na mfumo wa maisha yake, akijitahidi kukumbatia utakatifu wa maisha.

Yohane Mbatizaji anatangaza ujio wa Masiha atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa njia ya Maji ya Ubatizo, watu wanafanyika kuwa ni Watoto wa Mungu na hivyo kustahilishwa kushiriki katika matunda ya ahadi zilizotolewa wakati wa Agano kati ya Mungu na Waisraeli.

Kardinali Angelo Scola anasema, Kipindi hiki cha Majilio kwa namna ya pekee kabisa, kinaendeleza Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, sanjari na Uinjilishaji Mpya unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kufunga Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya alikumbusha kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wanaohitaji Kuinjilishwa Upya; Yaani wana kiu na njaa ya kutaka kukutana na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ili aweze kufungua macho yao pamoja na kuwafundisha njia wanayopaswa kuifuata katika hija ya maisha yao baada ya kumezwa na malimwengu, kiasi kwamba, ule moto wa Mungu uliokuwa umewashwa ndani mwao, unaonekana kuzima.

Watu wanahitaji kupata joto la Habari Njema ya Wokovu, kwa ajili yao wenyewe pamoja na Familia zao. Moto wa Imani uliowashwa miaka kadhaa iliyopita, unaendelea kufifia, hatari kwa waamini wanaoishi katika ulimwengu mamboleo! Kumbe, Uinjilishaji Mpya ni dhamana ya Wakristo wote.

Kardinali Angelo Scola anabainisha kwamba, Imani ni jibu makini kwa mahangaiko ya watu wa nyakati hizi. Kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuhakikisha kwamba, kila mtu anauona wokovu, ili hatimaye, aweze kukombolewa kwa njia ya Yesu Kristo, anayewaonjesha upendo na huruma ya Baba yake wa mbinguni.

Kuna maovu yanayoendelea kutendeka hapa duniani. Ikumbukwe kwamba, haki na huruma ni chanda na pete. Msamaha wa Mungu ni jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anatenda ili kumwokoa mwanadamu kutokana na mapungufu yake yaliyopita, kwa kutambua kwamba, anapaswa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, Mungu alimuumba mwanadamu pasi na ridhaa yake, lakini hawezi kumkomboa bila ushiriki wake.

Waamini wakati huu wa Kipindi cha Majilio, watambue mapungufu na dhambi zao, wakimbilie huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kama njia ya kujiandaa kumpokea Masiha na Mkombozi anayekuja Ulimwenguni.








All the contents on this site are copyrighted ©.