Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Majilio
Mpendwa mwana wa Mungu, Mama Kanisa daima akiongozwa na Roho Mtakatifu daima haachi
kutuwekea vipindi kwa ajili ya kujitakatifuza na kuongoza maisha yetu tukimwelekea
Mungu zaidi na zaidi. Tunamshukuru Mungu kwa upendo wake anaotujalia kwa njia ya Kanisa.
Tulimaliza
mwaka wa Kanisa vizuri na sasa tunaanza mwaka mpya wa Kanisa yaani mwaka C. Kumbe
leo ni Dominika ya kwanza ya Majilio, Dominika ambayo hufungua mwaka mpya wa Kanisa.
Ni Dominika ambayo hufungua kipindi cha Dominika 4 kwa ajili ya matayarisho ya Ujio
wa Masiha na Mkombozi yaani kuzaliwa Mtoto Emanueli aliye Mwana wa Mungu.
Katika
Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio na zaidi kipindi chote cha Majilio ujumbe
wa Neno la Mungu ni kuhusu kutayarisha njia ya Bwana. Tutakutana na Nabii Yeremia
ambaye mafundisho yake yanakazia timizo la ahadi za Mungu alizoweka kwa Wana wa Israeli.
Ahadi yenyewe ni ile yakwamba atawapelekea mfalme ambaye atazaliwa katika kiti cha
Daudi. Mungu hatoi ahadi tu ya kuwapelekea Mfalme bali Mfalme huyu atakuwa mfalme
wa haki na amani, atawatawala kwa unyofu wa hali ya juu. Ahadi hii ya Mungu inatimia
anapozaliwa Yesu Kristu Masiha katika ukoo wa Daudi.
Mpendwa unayenisikiliza,
dhamira kuu ya majilio ni matayarisho kwa ajili ya kumpokea Mkombozi, kumbe, matayarisho
hayo yanajikita katika kujiweka tayari kiroho na kwa namna hiyo dhihirisho likiwa
matendo mema daima katika jumuiya zetu. Matayarisho ni kutenda mapenzi ya Mungu, ni
kupendana na kuheshimiana na kuishi kidugu.
Matayrisho kadiri ya Mwinjili
Luka ni pia kuacha mambo ya zamani na kuishi maisha mapya. Kielelezo cha maisha ya
zamani ni ulevi, anasa na shughuli nyingine za kidunia zisizojenga ufalme wa Mungu.
Kwa kuacha maisha ya zamani tunajiweka tayari ili Bwana ajapo atukute tu tayari kwa
kunyakuliwa naye.
Ewe ndugu yangu unayenisikiliza siraha ambayo Mwinjili anatupatia
ni maisha ya SALA. Sala ni maongezi na Mungu na hivi kila asaliye hukaa karibu na
babaye na kwa jinsi hiyo ajapo hawezi kukuta hayuko tayari. Mtume Paulo anapowaandikia
Wathesalonike anawaasa kujiunda katika fadhila ya kupendana kati yao na kwa njia hii
watakuwa tayari kumlaki Bwana wakati ajapo.
Mpendwa mwana wa Mungu mafundisho
haya ni kwa ajili yetu hivi leo, yaani tunapaswa kujenga familia iliyosimama katika
msingi wa maelewano na mapendo kina. Kipindi cha majilio ni kipindi cha kupanda mbegu
bora ya uaminifu, utii, matumaini ili mwishoni tuvune tunda moja zuri nalo ni kupokea
mwanga wa milele, yaani uzima wa milele. Majilio yatudai kupokea sakramenti, kushiriki
Misa takatifu, kuwatembelea wagonjwa, kukesha katika sala na mambo yote mazuri yanayokusudia
kusimika ufalme wa Mungu.
Nikutakie maisha na majilio njema na kipindi chema
cha maandalizi ya Noeli na mwaka mpya. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa
kwako na Pd. Richard Tiganya cpps