Miaka sitini na tano imekwisha yoyoma tangu Umoja wa Mataifa ulipopitisha Azimio namba
181 lililogawanya Israeli na Palestina, anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana
Ban Ki-Moon katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Mshikamano wa Kimataifa
na Palestina, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Novemba.
Anasema,
Palestina bado inaendelea kukabiliana na hali ngumu ya maisha pamoja na vikwazo mbali
mbali, hii yote ni kutokana na Jumuiya ya Kimataifa kushindwa kutoa suluhu ya kudumu
kutokana na kinzani hizi.
NI matumaini ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
kwamba, Mataifa haya mawili yatajitahidi kukoleza utashi wa kisiasa; ari na moyo wa
ujasiri, kila upande ukiwajibika kupania kujenga na kudumisha amani ya kudumu kati
ya nchi hizi mbili ambazo zimekuwa zikisigana mara kwa mara wakiwa na matumaini kwa
vijana wa kizazi kipya. Majadiliano ya kina ndiyo dawa pekee ya amani, utulivu na
usalama huko Mashariki ya Kati.
Nchi hizi mbili zijitahidi kudhibiti biashara
haramu ya silaha; kubomoa ukuta unaowatenganisha pamoja na kuharakisha mchakato wa
upatanisho miongoni mwa Wapalestina. Serikali ya Palestina inawajibika anasema Katibu
mkuu kujenga miundo mbinu itakayorahisisha utekelezaji wa shughuli zake, daima ikijitahidi
kuheshimu Sheria za Kimataifa. Haki, Amani na Utulivu ni nguzo muhimu kwa ajili ya
ustawi wa Wananchi wa Palestina.