2012-11-30 08:35:12

Palestina sasa ni Taifa huru!


Umoja wa Mataifa, Alhamisi tarehe 29 Novemba 2012 umepitisha kwa kura nyingi Azimio linaloitambua Palestina kuwa ni nchi huru, ingawa bado inakabiliana na matatizo na changamoto nyingi; kwani hadi sasa haiwezi kudhibiti mipaka, anga wala biashara wala haina Vikosi vya Ulinzi na Usalama Kitaifa.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema huu ni ushindi mkubwa kwa Palestina katika Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, Rais Mahmoud Abbas amepewa dhamana ya kuunda Serikali katika maeneo ya Wapalestina. Hii ni hatua ya kwanza, kwani Palestina bado inapaswa kuendelea kufanya majadiliano ya amani na Israeli. Wapalestina wengi wameshangilia kutokana na uamuzi huu wa Umoja wa Mataifa kuwatambua kuwa ni nchi huru. Palestina inakuwa ni nchi mtazamaji wa kudumu wa Umoja wa Mataifa, kama ilivyo Vatican.

Itakumbukwa kwamba, kunako Mwaka 1947 Baraza kuu la Umoja wa Mataifa liliazimia kuigawa Palestina katika Mataifa mawili: Taifa moja kwa ajili ya Waisraeli na jingine kwa ajili ya Waarabu. Israeli ikawa ni nchi huru, lakini Palestina ikaendelea kutawaliwa, ikiandamwa na migogoro, vita na kinzani za kisiasa na kijamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.