2012-11-29 08:04:41

Mchango wa Kanisa Katoliki katika mapambano dhidi ya Umaskini na Deni la Nje Duniani



Mama Kanisa kwa miaka mingi amekuwa mstari wa mbele katika mchakato unaopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili; mikakati inayojionesha kwa namna ya pekee katika shughuli za kichungaji. Kwa namna ya pekee, Kanisa lilioneka kuguswa na matatizo yaliyokuwa yanajitokeza ndani ya Jamii wakati wa Mapinduzi ya Viwanda Barani Ulaya. Hapo, Papa Leo wa kumi na tatu, akaandika Waraka wa Kichungaji kuhusu Mambo Mapya, Rerum Novarum. RealAudioMP3

Huu ni Waraka ambao wachunguzi wa mambo ya kijamii wanasema kwamba, ni msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Paulo wa sita, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili na Benedikto wa kumi na sita, ni viongozi wa Kanisa ambao wameshuhudia na kuguswa na umaskini wa watu wengi zaidi duniani, kiasi cha kuamua kulivalia njuga suala zima la: umaskini na deni kubwa la nje ambalo limeendelea kuwatumbukiza watu wengi katika baa la umaskini pamoja na kudumaa katika maendeleo: kiroho na kimwili.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika kumbu kumu ya maadhimisho ya Miaka 20 ya Waraka kuhusu Mambo Mapya, aliandika Hati nyingine ya kichungaji inayobainisha uhusiano wa dhati uliopo baina ya deni la nje na baa la umaskini duniani. Mikopo anasema Papa Paulo wa Sita, katika Waraka wake juu ya Maendeleo ya Watu, inapaswa kuwa ni kichocheo cha maendeleo, lakini kwa bahati mbaya, imegeuzwa kuwa ni chombo cha kuwanyonya na kuwanyanyasa wananchi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, nchi ambazo zimekopa zinajikuta zikilazimika kulipa deni kwa fedha nyingi ambazo zimewekewa pia riba, fedha ambazo zingetumika katika kuchochea maendeleo ya watu; matokeo yake ni kwamba, watu wanazidi kudidimia katika lindi la umaskini siku hadi siku na wala hawaoni matokeo ya mikopo iliyotolewa kwa nchi zao

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anasema, kimaadili deni ni lazima lilipwe, hapa hakuna cha salia mtume! Lakini anasema kwamba, kuwalazimisha watu kulipa deni hili wakati wanaendelea kutumbukia katika dimbwi la umaskini na hali ya kukata tamaa ni jambo ambalo kimsingi ni kinyume kabisa cha maadili. Hali hii inahitaji tafakari ya kina na njia mbadala ili kuweza kila upande kutekeleza wajibu wake, kwa kutambua kwamba, wananchi wana haki ya kuoneshwa mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanuni auni katika harakati za kujitafutia maendeleo endelevu.

Wazo hili likavaliwa njuga na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, sanjari na maadhimisho ya Jubilee kuu ya miaka elfu mbili ya Ukristo, akayataka mataifa tajiri duniani kufuta deni la nje kwa nchi changa zaidi, ili fedha ile itumike katika maboresho ya huduma ya elimu, afya na maendeleo ya watu.

Mababa wa Sinodi ya Afrika, kunako mwaka 1994 wakaligusia tatizo hili tena na Papa Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji, Kanisa Barani Afrika, akaonesha masikitiko ya Mama Kanisa kutokana na mzigo wa deni la ndani na nje kwa nchi maskini duniani.

Akawasihi wakuu wa nchi kutowatwisha wananchi wao mzigo w a madeni ambayo hawataweza kuyalipa kamwe! Akazitaka taasisi za fedha kimataifa na nchi ambazo zimetoa mikopo kufuta deni lao kwa nchi changa duniani, changamoto ambayo ilifanyiwa kazi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, na matokeo yake yanaonekana!

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amerika, alikubaliana kimsingi na Mababa wa Sinodi kwamba, deni la ndani na nje, ni suala nyeti linalohitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Madeni haya mara nyingi ni matokeo ya: rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi. Ni matunda ya utawala mbovu wa watu wanaojitafuta wenyewe bila ya kujali mafao ya wengi.

Ni suala nyeti linalowagusa wale wanaotoa mikopo hii kwani mara nyingi ni watu na taasisi ambazo zimejaa tamaa ya kutaka kupata faida kubwa kwa gharama na mahangaiko ya watu wengine kutokana na riba kubwa wanayoiweka kwenye mikopo hii. Matokeo yake ni kwamba, mikopo inatumika kwa ajili ya kujaza mifuko ya watu wachache ndani ya Jamii, wakati ambapo kuna umati mkubwa watu unateseka na baa la umaskini na maendeleo yanazidi kudumaa na kusinyaa siku hadi siku.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anasema, kuwalipisha watu ambao hawakufaidi matunda ya mikopo hii ni jambo ambalo ni kinyume kabisa cha haki. Ikumbukwe kwamba, hata ile riba inayopaswa kulipwa inaondoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingeweza kutumika katika maboresho ya elimu, afya na maendeleo ya watu sanjari na kutoa fursa za ajira. Deni la nje, lilikuwa linawatesa wananchi wengi wa Amerika ya Kusini, kama anavyo bainisha Papa Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji, Kanisa Barani Amerika.

Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, ulikuwa ni muda muafaka wa kufuata madeni kwa nchi changa. Kanisa likashirikiana na wataalam bingwa katika masuala ya kichumi, deni likafutwa. Mwaka 2001, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, akawashukuru wote walioonesha tendo hili la ukarimu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee kuu mintarafu Maandiko Matakatifu. Ni kielelezo cha haki na mshikamano unaozingatia misingi ya maadili na utu wema.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, akaendelea kuhimiza matumizi bora na sahihi ya fedha za mikopo kwa kuhakikisha kwamba, mikopo hii inawanufaisha watu wengi ndani ya Jamii, ili kupata maendeleo ya kiuchumi na kisiasa. Suluhu ya tatizo hili inapaswa kuwa ni endelevu, kwa njia ya ushirikiano na mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni, ili fedha hizi zisaidie katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na baa la njaa duniani.

Ulipaji wa deni la nje uligeuza mwelekeo na badala ya kulipa fedha, nchi na mashirika na makampuni ya kimataifa yakadai yalipwe kwa njia ya malighafi inayohitajika viwandani au kupewa fursa za kuwekeza; kweli uchumi wa nchi nyingi ukacharuka, madini yaliyokuwa ardhini yakachimbuliwa, misitu iliyokuwa inapamba uso wa nchi ikakatwa, matokeo yake, wawekezaji kutoka nchi za nje wameondoka na rasilimali na utajiri wa nchi nyingi, wenyeji wameambulia mikataba tenge na mashimo makubwa ya machimbo ya madini.

Kumeibuka matabaka katika nchi hizi, matajiri wenye “vijisenti vyao” na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi, wanaolala macho wazi kama bundi, kwani kila kukicha ni afadhali ya jana! Kinzani na migogoro ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ikafumuka, vita ikaanza kupamba moto! Maskini wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini; matajiri "wanapeta kwa raha zao wenyewe"!

Hapa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, anakumbukwa kwa namna ya pekee, kwa kuhimiza misingi ya maadili na utu wema katika matumizi ya rasilimali ya nchi. Donda na balaa la umaskini likakuzwa kwa kiwango kikubwa na utandawazi, vita pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Anasema, kuna haja ya kuendeleza juhudi za kupambana na baa la umaskini duniani, kwa kukuza na kuimarisha maendeleo ya watu sanjari na kushughulikia deni la nje, kuwa ni kati ya vipaumbele vinavyopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya Kimataifa.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameendeleza changamoto hii iliyokuwa imevaliwa njuga na mtangulizi wake, kwa kuzisihi nchi tajiri zaidi duniani kufuta deni kwa nchi changa duniani, kwani hii nidhamana ya kimaadili, inayopaswa kutekelezwa na Familia ya binadamu, inayosimikwa katika utu wa pamoja katika mchakato mzima wa utandawazi. Mazungumzo ya Doha kuhusu kufutwa kwa deni la nje kwa nchi maskini zaidi duniani, yakakwama mchangani.

Deni la nje na umaskini ni mambo ambayo yana uhusiano wa karibu, yanahitaji nidhamu, maadili na mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni, ili kupata suluhu ya kudumu, kila mtu akitekeleza dhamana yake, jambo hili linawezekana.

Makala hii imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S na kusomwa kwako na Sr. Gisela Upendo Msuya.








All the contents on this site are copyrighted ©.