Kenya: Askofu ahimiza uinjilishaji kupitia vyombo vya mawasiliano.
Askofu Emmanuel Barbara (OFM), wa Jimbo Katoliki la Malindi Kenya , amehimiza waamini
Katoliki, kuvitumia vyombo vya habari kueneza Ujumbe wa Habari njema ya Injili.
Himizo
hili alilitoa wakati wa kuzindua warsha ya Kijimbo, iliyofanyika katika Kituo cha
Kichungaji cha Malindi, Ijumaa iliyopita Novemba 23 , na kuhudhuriwa na wanahabari
kutoka Jimbo la Malindi na Jimbo Kuu la Mombasa.
Jimbo kuu la Mombasa hujumuiya
majimbo Katoliki ya Malindi, Mombasa na Garissa, Katika warsha hii, wanahabari kutoka
jimbo la Garissa hawakuhudhuria kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo lao lililotajwa
kuwa katika hali ya hatari na hivyo watu wamekatazwa kutembea ovyo.
Wakati
wa Warsha Askofu Barbara, alivitaja vyombo vya mawasiliano kuwa na uwezo mkubwa wa
kuwaunganisha watu, kama inavyoonekana sasa kwamba, vimewezesha dunia kuwa kijiji
kidogo na kujenga umoja na mshikamano zaidi kati ya watu. Kwa manufaa hayo, pia vinaweza
kutumika katika kueneza haraka Neno la Mungu.
Alisema, hii ni njia inayofaa
kueneza haraka ujumbe wa Injili kwa watu wote. Na hasa Redio, inao uwezo wa kupenyeza
ujumbe kwa familia nyingi bila lazima ya kuonana ana kwa ana na familia, hasa zilizoko
katika maeneo ya ndani vijijini na pia maeneo hatarishi. Na hivyo njia hii ya redio
inarahisisha kazi ya kuinjilisha.
Askofu Barbara, alieleza na kutaja jinsi
Baba Mtakatifu Benedikto XV1, alivyojiunga na tovuti ya Facebook na hivyo kuliinua
jukwaa la wanahabari wa kanisa katika uwanja mpya wa mawasiliano.
Na aliitaja
changamoto inayowakabiliwa wanamawasiliano wa Kanisa , ni kufika katika vyombo vya
habari, na kuanzisha mijadala juu ya amani na ukweli.