Kwa nini umaskini? Hili ni swali msingi ambalo Shirikisho la Watangazaji
Ulaya, “European Broadcasting” EBU linawaalika watu kulitafakari kupitia
vyombo mbali mbali vya habari, hapo tarehe 29 Novemba 2012. Umaskini ni jambo la zamani,
lakini linafumbata mambo mapya kwa sasa. Kuna wakati ambapo watu wengi waliufumbia
macho umaskini sehemu mbali mbali za dunia; lakini leo hii, wananchi wanaoishi katika
Nchi Tajiri zaidi duniani, wanachangamotishwa na Serikali zao pamoja na Mashirika
ya Fedha Kimataifa kujifunga mikanda ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha.
Huu
ndio ule wimbo uliombwa kwenye miaka 80/90 kwa nchi nyingi za Kiafrika, walipoambiwa
kujifunga mkanda, kiasi kwamba, baadhi ya nchi kama vile Msumbiji wakasema, kwa hakika,
watu wanapoteza maisha yao kutokana na masharti magumu ya kiuchumi yanayotolewa na
Taasisi za Fedha Kimataifa.
Katika kipindi cha Mwaka 1994, uwezo wa kununua
bidhaa na huduma kwa wananchi wanaozungumza lugha ya Kifaransa, ukashuka kwa asilimia
50%; matokeo yake, mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma ikapaa juu maradufu! Wakasema,
ni matokeo na athari za Ukoloni. Wananchi hawa ambao wamekuwa sugu kutokana na umaskini
na hali ngumu ya maisha kutoka katika Nchi Maskini duniani, kilio chao hakikusikilizwa,
ikawa ni sawa na machozi ya Samaki kuishia majini.
Takwimu zinabainisha
kwamba, kati ya nchi 44 Maskini zaidi duniani, kati yake nchi 33 zinapatikana Barani
Afrika. Umaskini huu wanasema kwamba, ni matokeo ya: utawala mbaya, udikteka, vita,
kinzani na migogoro ya kikabila; mgawanyo na matumizi tenge ya rasilimali ya nchi;
rushwa na ufisadi; wasomi wengi kukimbia nchi zao kwa kutafuta malisho ya kijani kibichi
ughaibuni; uhusiano tenge wa shughuli na mikakati ya kiuchumi na nchi za Bara la Afrika;
ukwapuaji wa malighafi toka Barani Afrika; ukoloni na athari zake. Hali hii pia inajitokeza
katika Nchi za Amerika ya Kusini na Asia, ambazo zilipachikwa jina na kuitwa Nchi
Zilizoko Dunia ya Tatu, “LDC”.
Wasomi wengi waliangalia mwenendo huu
wa uchumi kwa macho ya makengeza, kwani kuwa watu waliokuwa wanaishi katikati ya dunia
na wengine walisukumizwa pembezoni kabisa mwa dunia; lakini bado zikaendelea kutegemeana
katika uwiano tenge, kiasi cha kuanza kuibua hisia ya kutaka uwepo Mfumo Mpya wa Uchumi
Kimataifa, “NIEO”, bila shaka wachumi wengi watakumbuka mwenendo huu,
lakini wazo hili halikuweza kufanyiwa kazi, ili kuleta uwiano bora na tengamanifu
katika masuala ya kiuchumi. Ndiyo maana EBU linauliza tena leo hii “Kwa nini Umaskini?”
Hapa
tunazungumzia umaskini wa hali na kipato, unaoendelea kugusa mamillioni ya watu kutokana
na kukoswa fursa za ajira katika Nchi ambazo, hadi siku za hivi karibuni, zilijulikana
kama Nchi Tajiri Duniani; mahali ambapo watu walikuwa kuku kwa mrija! Wananchi kutoka
Afrika, Asia na Amerika ya Kusini, wakaendelea kuambulia pakavu! Umaskini wa kiuchumi
ni chanzo cha mtikisiko huu, ambao pia umechangiwa na mambo mengine msingi katika
maisha ya mwanadamu.
Kwa miaka mingi Kanisa lilihimiza maendeleo endelevu yanayogusa
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kitamaduni na kijamii. Mtu na utu wake hana
budi kuwa n ikiini cha mikakati ya maendeleo, vinginevyo ni kupoteza dira na hatimaye,
kukosa mwelekeo. Kanisa liliona na kutambua madhara na hatari katika maisha ya kijamii,
kwenye uchumi uliokuwa unakumbatia mfumo wa Ubepari uliokuwa unajikita katika faida
kubwa, pasi ya kujali misingi ya maadili na utu wema! Matokeo yake ni kilio kinachoendelea
kusikika kutoka sehemu mbali mbali za dunia baada ya kuguswa na makali ya kuchechemea
kwa uchumi wa kimataifa!
Haya ni matokeo ambayo baadhi ya wanazuoni kutoka
Afrika kama vile Engelbert Mveng wanauita ”Umaskini wa Kiutu”, yaani ni umaskini
ambao umemtikisa mwanadamu katika undani wa maisha yake; katika jinsi ya kufikiri
na kutenda; katika kujiwekea mikakati yake kwa siku za usoni. Wale ambao walidhani
kwamba wameupatia umaskini kisogo, leo hii wanaguswa na kutikiswa vibaya sana, kwa
sababu binadamu wote ni sawa! Waswahili wanasema, eti kutesa kwa zamu! Kama
anavyokiri pia C. Hamidou Kane katika kitabu chake kijulikanacho kama ”L’aventura
Ambigua”
Kuna haja ya kuweka uwiano bora zaidi kati ya nchi zilizoendelea
na maskini zaidi duniani, kwa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na ugavi bora wa rasilimali
ya dunia unaozingatia msingi wa haki na mshikamano unaoongozwa na kanuni. Watu wanapaswa
kujifunza kuwa na kiasi na kwamba, hata katika umaskini, bado watu wanaweza kuthamini
utu na heshima ya mwanadamu.
Hii ni changamoto iliyokuwa imetolewa kunako
mwaka 1978 na Albert Tèvoèdjirè katika kitabu chake ”La povertà, Ricchezza dei
Popoli” Huu ni umaskini jeuri, unaomwezesha mtu kuthamini utu na heshima yake
na kwamba, mali si kipimo cha utu; mwaliko wa kutumia utajiri nam ali ya dunia kama
kielelezo cha mshikamano wa upendo na ”akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, wanaoendelea
kuongezeka siku hadi siku! Kila mtu atambuliwe, aheshimiwe na kuthaminiwa.
Huu
ndio muhtari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa unaojikita katika Kweli za Kiinjili na
kwamba dunia itapita, lakini Neno la Mungu litabaki Imara. Mtikisiko wa uchumi kimataifa,
uikumbushe Jumuiya ya Kimataifa kwamba, wote wanasafiri katika mtumbwi mmoja kama
binadamu, kwa kushikamana kwa pamoja, wanaweza kuokoka, lakini kila mtu akijitafuta
mwenyewe, matokeo yake ni kuangamia. Watu waufahamu umaskini na changamoto zake, pengine
ni huduma makini ambayo EBU imetoa kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuuliza swali msingi
”kwanini umaskini”?
Tahariri hii imeandaliwa na Dr. Maria Dulce Araujò Evora
kutoka Idhaa ya Kireno ya Radio Vatican na kutafsiriwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.