Mawaziri wa mambo ya ndani ya nchi wanajadili mkakati wa kufuta Adhabu ya Kifo! Hakuna
haki pasi na maisha!
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeandaa Kongamano la Saba la Kimataifa linalowashirikisha
Mawaziri wa Mambo ya ndani ya nchi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaojadili
kuhusu adhabu ya kifo, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Dunia pasi na adhabu ya kifo;
hakuna haki pasi na maisha".
Haki na maisha na dhana zinazokwenda sanjari,
changamoto kwa wanasiasa wanatekeleza dhamana hii katika sera na mikakati yao kuhusu
utekelezaji wa misingi ya haki ndani ya Jamii. Hadi sasa kuna nchi 150 ambazo zimefuta
katika sheria zake utekelezaji wa adhabu ya kifo, kama kielelezo cha kutaka kuenzi
haki msingi za binadamu.
Wataalam wanabainisha kwamba, adhabu ya kifo ni kielelezo
cha hali ya juu cha uvunjaji wa haki msingi za binadamu; jambo ambalo linakwenda sanjari
na ubaguzi unaofanywa katika mifumo mbali mbali ya maisha ya binadamu. Idadi kubwa
ya watu wanaohukumiwa adhabu ya kifo ni maskini! Watu wenye fedha zao, wanaweza kujitetea
na hatimaye kuepuka adhabu ya kifo, lakini maskini, watakiona cha mtema kuni.
Takwimu
nchini Marekani ambako adhabu ya kifo inaendelea kutekelezwa zinaonesha kwamba, kati
ya kesi 15,978; wazungu wapatao 30 tu ndio waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, wakati
ambapo 15948 kutoka katika makundi mbali mbali walipatikana na hatia ya kunyongwa
hadi kufa! Kuna makosa ya kisheria yanayofanyika na matokeo yake watu wasiokuwa na
hatia wanajikuta wamenyongwa na haki yao kupotea kabisa.
Bi Theresa Makone
anasema, nchini Zimbabwe, adhabu ya kifo haijawahi kutekelezwa kwa kipindi cha miaka
32, hali inayoonesha kwamba, kuna haja ya kufanya marekebisho ya sheria ili kufuta
adhabu ya kifo nchini humo. Falsafa ya jicho kwa jicho ni hatari kwani nchi inaweza
kujikuta ikiwa na vipofu wengi. Kwa hakika, adhabu ya kifo ni kitendo kinachopingana
na utu wema pamoja na haki msingi za binadamu.
Hiki ni kielelezo cha watu
kutaka kulipizana kisasi, jambo ambalo kamwe halina tija wala maendeleo kwa Jamii
husika. Kutokana na changamoto hizi, kuna haja kwa Wanasiasa na Jamii kwa ujumla,
kusimama kidete kupinga adhabu ya kifo, kwani Jamii haiwezi kuongozwa kwa msingi wa
hofu na kwamba, magereza yamekuwa ni maeneo ya taabu na mahangaiko ya watu wengi wasiokuwa
na hatia, jambo ambalo haliwezi kuvumilika. Kuna haja ya kutafuta njia mbadala dhidi
ya adhabu ya kifo!