Kardinali Polycarp Pengo anawahimiza Wanawake Wakatoliki kumwilisha upendo kwa vitendo!
Ifuatayo ni hotuba ya Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es
Salaam, wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, yaliyofanyika
hivi karibuni Jimbo kuu la Dar es Salaam, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu
WAWATA ilipoanzishwa.
Mhashamu Askofu Mkuu Francisco M.Padilla Balozi wa Baba
Mtakatifu Nchini Tanzania. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma –Mwenyekiti wa Idara
ya Utume wa Walei katika Baraza la Maasfofu Katoliki Tanzania. Waheshimiwa Mapadre,
Watawa wa kike na wakiume Waheshimiwa Viongozi Mbalimbali wa Serikali na Taasisi Wageni
Waalikwa toka Kenya, Uganda, Malawi na Zambia Wapendwa mama zangu WAWATA.
Adhimisho
la Miaka 40 ya WAWATA ni tendo ambalo limelifurahisha sana Kanisa katika ngazi zote
kwa sababu limetoa fursa ambapo WAWATA kwa namna ya pekee mumeweza kutafakari Utume
wenu katika kanisa na jamii hasa mkijikita katika kauli mbiu ya adhimisho la miaka
40 ya WAWATA “Upendo kwa Vitendo”Katika harakati zenu za ujumla za kutumikia kwa Upendo
wa Kristu.
Kanisa zima la Tanzania linawapongeza sana kwa hatua mliyofikia
na kuwaasa kwamba tafakari mlizofanya katika ngazi zote kwa kipindi chote ziwe chachu
ya kuongeza juhudi na kuwajibika zaidi awamu nyingine za miaka ijayo baada ya adhimisho
hili.
Nimefurahishwa binafsi na kujifunza mengi sana kutokana na maonesho
ambayo mmenipa fursa ya pekee ya kuyafungua. Nimejionea mwenyewe mambo mbalimbali
ambayo ni vielelezo vya kazi ya Mwanamke Mkatoliki katika nyanja za kujiendeleza
kiroho na kimwili hususani ; Uchumi, malezi ya watoto na vijana , utunzaji wa, mazingira,
elimu ya dini n.k kwa kuzingatia Kauli mbiu ya WAWATA ya “Kwa Upendo wa Kristu Tutumikie
na Kuwajibika”
Mnafanya kazi nzuri ambazo ni kwa ajili ya maendeleo ya kanisa
na jamii kwa ujumla. Umoja wenu unajitahidi kuwafanya WAWATA wajitakatifuze; ili
waweze kuyatakatifuza malimwengu kazi ambayo kwa ubatizo wenu mmeitwa kufanya. Ushiriki
wenu katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni muhimu sana katika kuyatakatifuza malimwengu
kwani kwa kupitia Jumuiya Ndogo ndogo zinazowajibika ,ndipo tunapata familia bora
zenye kutoa viongozi bora wa kanisa na taifa.
Munashiriki harakati mbalimbali
za kujikomboa kiuchumi k.m: kuondokana na umaskini,unyanyasaji, maradhi ili kwa
kujikomboa kwenu muwakomboe wengine na kuwa chachu ya maendeleo kuanzia ngazi ya
familia hadi taifa . Kanisa limeshuhudia mkianzisha na kutekeleza miradi mbalimbali
katika vikundi vyenu, vigango, parokia majimbo, n.k. Uongozi unaowajibika,na uaminifu
katika kutekeleza hayo yote ni muhimu sana ili shughuli hizo zote ziwe endelevu na
kuleta mabadildiko yenye kuwanufaisha walengwa na jamii kwa ujumla.
Aidha nimefurahi
sana kuona mmetenga muda wa kujadili na kutoa maoni yenu kuhusiana na marekebisho
katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania. Ni jambo Muhimu sana kwani ni wajibu wenu
kufanya hivyo hivyo nawahimiza mushiriki kikamilifu mchakato huo katika ngazizake
zote .
Mnapotafakari kauli mbiu ya “Upendo kwa Vitendo” Mnafahamu Yesu Kristo
mwenyewe alitudhihirishia Upendo wa Mungu kwa maisha yake yote. Ndiyo maana alisema:
“Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki
zake”. (Yohane 15:13.) Alionyesha haya katika kuwafundisha wafuasi wake kwa hali
na mali. Aliwaponya wagonjwa, viwete vipofu, viziwi na bubu n.k. Aliona shida za
watu akajali na kuwajibika katika kuwahudumia bila kutafuta faida.
Dunia ya
leo inahitaji sana upendo ili amani na ustawi viweze kushamiri. Hivyo WAWATA na wanawake
kwa ujumla ambao ni wa kwanza katika dhamana ya uhai wa bianadamu wana nafasi ya pekee
katika jamii.Hivyo natoa mwito kwa dhati kabisa kuwa pandeni mbegu za upendo kwanza
katika familia iliyo shule ya kwanza ili watoto wote waonje upendo wa baba na mama
na hivyo waweze kuiga na kuwa raia wema. Hivyo mtakapondaa mkakati wa shughuli za
WAWATA katika kipindi kijacho.
Zingatieni sana malezi yenye kujenga upendo
katika familia ili kizazi kijacho kiwe na amani na ustawi zaidi .Mwito huu ni kwa
ajili ya wazazi wote yaani baba na mama pamoja na wale wote wanaohusika na malezi
ya wataoto na vijana katika jamii zetu walezi .Tuonyeshe Upendo kwa vitendo ili
kwa matendo yenu jamii iwatambue kuwa nyinyi ni wafuasi kweli wa Kristu!
Nawapongeza
sana kwa maadhimisho haya ya miaka 40 ya Umoja wenu WAWATA na nawatakia heri na
baraka katikasafari ya kuelekea mbele yenye kujituma zaidi.