Majaji wa Mahakama kuu waapishwa Ikulu, Dar es Salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu, Novemba 26, 2012 amewaapisha Majaji wawili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania. Katika sherehe
iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed
Chande Othman, Rais Kikwete amewaapisha Jaji Bethuel M.K. Mmilla na Jaji Ibrahim
Juma kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani.
Rais Kikwete aliwateua Majaji hao tokea
Oktoba 25, mwaka huu wa 2012, na kabla ya uteuzi wake, Jaji Bethuel M.K. Mmilla alikuwa
Jaji wa Mahakama Kuu kwa miaka kumi tangu Juni 02, 2002. Vile vile, Jaji Mmilla amekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kwenye vituo vya Sumbawanga, Arusha na Mbeya.
Naye
Jaji Ibrahim Juma kabla ya uteuzi wake alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria
tangu mwaka 2007 na pia Jaji wa Mahakama Kuu tangu Juni, 2009. Pia amewahi kuwa Mkuu
wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kati ya mwaka 2003 na mwaka 2006.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete amemwapisha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mheshimiwa
John Mkwawa kuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na amemwapisha Bi. Winfrida
Beatrice Korosso kuwa Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.