Jimbo Katoliki Mbeya linajiandaa kuadhimisha Sinodi ya Jimbo kwa kujikita katika Utume
wa Familia
Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania anatarajiwa kufungua Maadhimisho
ya Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, Januari, 2013 kwa kupania kujikita zaidi katika
Utume wa Familia. Waamini wataweza kupata nafasi ya kutembeleana nyumba hadi nyumba
ili kuimarisha Utume wa Familia, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbali mbali
kutoka ndani na nje ya familia yenyewe.
Askofu Chengula anabainisha kwamba,
Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, itakuwa ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu
maisha na utume wake mintarafu mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto iliyotolewa
na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, iliyohitimishwa hivi karibuni
mjini Vatican. Katika maadhimisho hayo, Jimbo Katoliki Mbeya, litazindua pia Mkakati
wa shughuli za kichungaji, ambao utakuwa dira na mwongozo wa Jimbo Katoliki Mbeya
kwa miaka kadhaa ijayo.
Kanisa linapenda kuimarisha imani miongoni mwa waamini
kwa kujikita zaidi katika masuala ya Maandiko Matakatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa
Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na kuendelea kutafakari kuhusu utajiri
mkubwa unaofumbatwa katika Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; changamoto
kwa waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha, sanjari na kuendeleza jitihada za Mama
Kanisa katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao amini.
Maadhimisho
ya Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, itakuwa ni fursa kwa Kanisa Jimboni Mbeya, kufanya
tathmini ya kina kuhusu: majadiliano ya kidini na kiekumene, ikizingatiwa kwamba,
Mbeya ni kati ya mikoa ambayo ina idadi kubwa ya madhehebu mbali mbali ya Kikristo,
pengine, kuliko sehemu nyingine yoyote ya Tanzania. Ni muda wa kukazia majadiliano
ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga na kuimarisha misingi ya: haki,
amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; daima wajikitahidi kutafuta mafao ya wengi.
Uchumi
na maendeleo ya Kijamii ni mada itakayochambuliwa mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa,
ikizingatiwa kwamba, leo hii kuna idadi kubwa ya watu wanaoendelea kutumbukia katika
baa la umaskini, ujinga na njaa na kwamba, hali inazidi kuwa mbaya hata kuliko ilivyokuwa
miaka kadhaa iliyopita! Hapa kuna haja ya sera na mikakati ya maendeleo kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Baada
ya Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo Katoliki Mbeya, Askofu Evaristo Chengula anatarajiwa
kutoa Waraka mara baada ya Sinodi, utakaokuwa ni dira na mwongozo wa Kanisa Katoliki
Mbeya katika mikakati yake ya shughuli za kichungaji na kitume! Ni mwaliko kwa Familia
ya Mungu Jimbo Katoliki Mbeya kushikamana na kutembea kwa pamoja, ili waweze kwa pamoja
kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.