CAFOD inaadhimisha Jubilee ya miaka 50 kielelezo cha mshikamano wa upendo
Shirika la Misaada na Maendeleo Kimataifa la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza,
CAFOD linaadhimisha Jubilee ya miaka hamsini tangu lilipoanzishwa, kielelezo makini
cha mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni kwa watu wanaokabiliwa na shida
mbali mbali duniani.
Shirika hili lilianzishwa kunako mwaka 1962 wakati wa
vugu vugu la maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini na watu wenye
mapenzi mema, wakaalikwa kwa namna ya pekee na Kanisa kufunga na kujinyima wakati
wa kipindi cha Kwaresima, ili kile kidogo walichojinyima, kiweze kukusanywa na kupelekwa
katika maeneo yaliyokuwa yanahitaji msaada zaidi.
Kunako mwaka 1967 Papa Paulo
wa sita, akaandika Waraka wa Kichungaji: Maendeleo ya Watu, Populorum Progressio.
Waraka huu kwa miaka yote hii, umekuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa CAFOD
sehemu mbali mbali za dunia. Mang’amuzi yake yameboreshwa zaidi na Nyaraka nyingine
zilizotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili: Sollicitudo rei socialis na Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Upendo katika Ukweli.
Hili ni Shirika
la misaada ambalo kimsingi linaongozwa na Imani ya Kanisa Katoliki inayofafanuliwa
katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kwa kipindi
cha miaka hamsini, CAFOD imeshikamana na wadau mbali mbali wa maendeleo kutoka Afrika,
Asia na Amerika ya Kusini, ili kukabiliana na majanga asilia, maafa na athari za vita,
kinzani na migogoro.
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, zaidi ya Sterling
za Uingereza Milioni arobaini na tatu zimetumika kwa ajili ya kugharimia misaada ya
maendeleo sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kukabiliana na majanga asilia na maafa
mbali mbali. Ni utume ambao unatekelezwa kwa kuwahusisha watoto na vijana ambao wanajinyima
ili kuchangia ustawi na maendeleo ya watu wanaokabiliana na umaskini, ujinga na maradhi.
Huu ni utamaduni wa upendo na mshikamano, unaojitahidi kumwilisha Injili ya
Upendo, kwa kuguswa na mahitaji ya jirani. Kwa maneno mengine, hii ni imani katika
matendo, inayopania kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Mikakati yake ya maendeleo
inamlenga mtu mzima: kiroho na kimwili, kwani wanatekeleza wajibu na dhamana hii kwa
kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kumletea mwanadamu maendeleo endelevu na ya
kudumu.
Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, mengi yamefanyika hususan
katika sekta ya afya, elimu, maendeleo endelevu, kilimo, uchumi. Wameendelea kuzihimiza
Serikali kusimamia utawala bora sanjari na kufuta deni la nje, ambalo kwa nchi nyingi
limekuwa ni kikwazo cha maendeleo endelevu. CAFOD katika mikakati yake, inapania kusimama
kidete dhidi ya umaskini na ukosefu wa misingi ya haki jamii, daima wakiongozwa na
Kweli za Kiinjili, kwani haya ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo katika majiundo
ya wafanyakazi na wanachama wa CAFOD.
Jubilee ya Miaka hamsini ya CAFOD ni
kipindi muafaka cha kuweza kufanya tathmini ya kina, kumshukuru Mungu kwa wema na
ukarimu aliowatendea pamoja na kuomba ulinzi na salama kutoka juu mbinguni, ili waendelee
kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa watu wanaoogelea katika
baa la umaskini, ujinga na maradhi.
CAFOD kwa sasa inakabiliwa na changamoto
nyingi kati ya hizi ni myumbo wa uchumi kimataifa na athari zake kwa mamilloni ya
watu sehemu mbali mbali za dunia; athari za mabadiliko ya tabianchi; njaa, ukame pamoja
na majanga asilia. Haya ni mambo yanayodumaza maendeleo ya watu. Jubilee ya miaka
hamsini ya CAFOD ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana na changamoto zote hizi,
ili hatimaye, kujega misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kimataifa unaoongozwa
na kanuni auni.
Mwaka wa Imani, uwe ni kipindi muafaka wa kuonesha Imani katika
matendo, ili kwamba, kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu aweze kuheshimiwa
na kuthaminiwa utu wake.